Saturday, February 16

Azam fc mguu mmoja ndani ya mzunguuko wa pili kombe la shirikisho; yaichapa Al Nasri ya Sudan Kusini mabao 3-1.


Kikosi cha timu ya Azam fc wana lambalamba.
AZAM FC, jana ilitanguliza hatua moja kwenye mstari wa kucheza raundi ya pili Kombe la Shirikisho baada ya kuitungua Al Nasri ya Sudan Kusini mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, sasa unakifanya kikosi cha Kocha Stewart Hall kuhitaji japo sare ya aina yoyote ili kusonga mbele hatua ya pili ya michuano hiyo.
Hata hivyo, pamoja na ushindi huo Azam inayocheza kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Caf, wangeweza kufunga mabao mengi zaidi hasa kipindi cha pili walichotawala mwanzo, mwisho, huku kipa wa Nasri Peter Midia akiwa kikwazo kikubwa.
Katika mchezo huo, Abdi Kassim alifunga mara moja kabla ya filimbi ya kutenganisha mchezo na Kipre Tchetche akaongeza mawili kipindi cha pili.
Kipigo hicho hakikuonekana kumshtua kocha wa Nasri, Ramzi Sebit kwani, mara baada ya mchezo alisema wanastahili kupata ushindi mnono mechi ya
marudiano.
“Nimeona upungufu wa wachezaji wangu, nakwenda kufanya marekebisho ili tushinde mechi ya marudiano,” aliwaambia waandishi wa habari.
Abdi alibadilisha ubao wa matokeo na kusomeka 1-0, baada mpira wake wa kichwa kulenga shabaha nyavu za Nasri kufuatia krosi ya Kipre Tchetche dakika ya 14.Nasri, ambao nao wanacheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya Sudan Kusini kujitenga na Khartoum, walisawazisha dakika ya 38 kupitia Fobian Elias kwa shuti.

Tchetche aliyekuwa mwiba ngome ya Wasudan hao, aliwafurahisha mashabiki waliojitokeza uwanjani kushangilia kwa kufunga bao la pili kwa kichwa dakika ya 80.
Kabla ya bao hilo, Tchetche alikaribia kufunga kama siyo mpira aliopiga kukosa shabaha na kugonga ‘paa’ la goli la Nasri dakika ya 54 kabla ya mabeki kuokoa.
Tchetche alikuwa hatari zaidi baada ya kuingia John Bocco kuchukua nafasi ya Abdi, alikaribia kufunga dakika ya 60, shukrani kwa kipa wa Nasri aliyefanya kazi nzuri. Bao la tatu la Azam lilikuja dakika ya 90 kupitia tena kwa Tchetche aliyefunga kirahisi akimalizia krosi ya Humphrey Mieno.
Kocha Hall, alisema amefurahishwa na matokeo hayo na kwamba anajipanga kufanya marekebisho kwenye safu ya kiungo kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
Aidha, katika hatua nyingine suala la uzalendo liliendelea kuwa ugonjwa nchini, kufuatia mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa Yanga kuishangilia Nasri iliyovaa jezi za njano.