Showing posts with label Kimataifa. Show all posts
Showing posts with label Kimataifa. Show all posts

Thursday, December 5

Mzee Nelson Mandela afariki dunia.

Tanzania imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia tarehe 6 hadi 8 Desemba, 2013, kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Rais Jakaya Kikwete wa nchi hiyo pia ameagiza kuwa katika kipindi hicho cha siku tatu bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

"Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na 21.Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri, mwana mapinduzi , mvumilivu na mstahimilivu". Ameongeza Rais Kikwete.Kufuatia kifo hicho Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na kupitia kwake kwa mkewe Bi Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi wote wa Afrika ya Kusini kufuatia kifo cha Mzee Nelson Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba, 2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Rais ameuelezea msiba huu kuwa ni msiba mkubwa kwetu sote.
Rais amemuelezea Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo uliomwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini kuwa taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
"Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa . Ni wajibu wa wana Afrika Kusini, Afrika na dunia kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake". Rais ameongeza kusema, "Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Mandela mahali pema peponi".
Mandela amefariki huko Johannesburg akiwa na umri wa miaka 95 na yeye ndiye aliyeiongoza Afrika Kusini kutoka mikononi mwa watawala wa ubaguzi wa rangi baada ya kufungwa jela kwa miaka 27.
Mandela alikuwa anatibiwa homa ya mapafu nyumbani kwake baada ya kulazwa hospitalini kwa miezi mitatu.
Katika taarifa yake kwa watu wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, alisema kuwa Mandela amewaaga lakini yuko mahali salama.
Rais Zuma amesema kuwa taifa limepoteza mtu waliyemjua kama mtoto wa taifa hilo.
Mandela aliwahi kushinda tuzo ya amani ya Nobel, na kutambulika kama rais aliyeheshimika sana hasa kwa kupatanisha watu wa Afrika Kusini baada ya kutoka gerezani.

Chanzo: bbc.

Tuesday, November 26

Bashar al-Assad hatahudhuria mazungumzo.

Fabius  amesema  hayo  siku  moja  baada  ya  Marekani na  Urusi  kuweka  uzito  katika  mazungumzo  hayo yaliyocheleweshwa  kwa  muda  mrefu, ambayo  Umoja  wa Mataifa  umesema  hatimaye  yatafanyika  Januari 22. Mpatanishi  wa  kimataifa  nchini  Syria  Lakhdar Brahimi amesema  orodha  ya  washiriki  haijapangwa. Msemaji  wa wizara  ya  mambo  ya  kigeni  Romain Nadal  amesema Ufaransa  inataka  pande  zote  kutuma  ujumbe  mmoja kila  mmoja.
Chanzo: DW 

Sunday, September 1

Obama aomba bunge kuidhinisha vita.

Haikuelekea kuwa Marekani itachukua hatua haraka ya kijeshi dhidi ya Syria, baada ya Rais Obama kuliomba bunge kuidhinisha shambulio.
Bunge halitaanza tena vikao hadi tarehe 9 September.
Mswada unaomba idhini ya bunge kutumia nguvu kuizuwia serikali ya Syria kutumia silaha za kemikali kwenye mashambulio.
Kuchelewa kwa ratiba ya Marekani piya kunawapa muda wakaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa kumaliza uchunguzi ndani ya maabara.
Wakaguzi hao wamerudi na sampuli walizopata kwenye eneo linalodaiwa kuwa lilishambuliwa kwa silaha za kemikali, karibu na Damascus.

Chanco: bbc

Friday, August 23

UN yataka uchunguzi kufanywa Syria

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limefanya kikao cha dharura kujadili madai kwamba wanajeshi wa serikali ya Syria wametumia silaha za kemikali pale walipofanya shambulio dhidi ya eneo lililopo nje kidogo ya mji mkuu wa Damascus hapo jana jumatano.
Wanaharakati wa upinzani wamesema kuwa mamia ya watu wakiwemo watoto wameuwawa huku muungano wa upinzani ukiyataja mauaji hayo ya halaiki. Serikali ya Syria imekanusha kwamba imetumia silaha hizo.
Mwenyekiti wa baraza la usalama, Maria Parceval, ambaye ni balozi wa Argentinean katika umoja wa mataifa amesema kuwa wanachama wa baraza hilo wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na madai hayo.
"Naweza kusema kuwa kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanachama wa baraza kuhusu madai hayo. Kuna hisia kwamba kuna haja ya kuwa wazi kuhusu kilichotokea na hali kufuatiliwa kwa makini,'' anasema Bi. Maria Parceval.
''Wanachama wote wanakubaliana kwamba matumizi yoyote ya silaha za kemikali, kwa yeyote katika mzozo huu, na katika mazingira yoyote ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Kulikuwa pia na makubaliano ya kutoa wito wa kusitishwa uhasama na vita.''
Kadhalika Bi. Perceval amesema kuwa kulikuwa na makubaliano kuhusu haja ya kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusiana na swala hilo.
''Wanachama wa baraza la usalama wametaka katibu mkuu aingilie kati ili kuhakikisha kuwa uchunguzi wa haraka na wa kina usioegemea upande wowote unafanywa. Wanachama wa baraza wameelezea haja ya kutolewa mara moja msaada wa kibinadamu kwa waathiriwa. Hatimaye baraza la usalama limetoa rambi rambi kwa waathiriwa pamoja na familia zao,'' ameongeza kusema Bi. Maria Perceval, mwenyekiti wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.


Chanzo: bbc

Tuesday, August 20

Zimbabwe iondolewe vikwazo, yasema SADIC.

Viongozi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wamezitaka dola za Magharibi kuondoa vikwazo vilivyowekewa nchi ya Zimbabwe, baada ya kuithinisha ushindi wa Rais Robert Mugabe.
Rais wa Malawi Joyce Banda ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Muungano wa SADC amesema raia wa Zimbabwe ndio wanaoumia na vikwazo hivyo.
Muungano wa Ulaya na Marekani ziliwekea Zimbabwe vikwazo mwaka wa 2002 baada ya kulalamikia utawala wa Mugabe kwa kuwakandamiza wapinzani wake. Hata hivyo Mugabe amekanusha madai hayo. Rais huyo wa Zimbabwe anatarajiwa kuapishwa upya Alhamisi ya wiki hii.
Tayari Mugabe na washirika wake tisa ambao ni maafisa wa chama tawala cha Zanu-PF wamewekewa vikwazo vya usafiri na Muungano wa Ulaya. Pia kampuni kadhaa zimepigwa marufuku kufanya biashara na Muungano huo.

Marekani pia imeweka vikwazo kwa Mugabe dhidi ya kuzuru nchini humo na kuharamisha kampuni shirika za Mugabe dhidi ya kufanya biashara na Washington.
Robert Mugabe alishinda Urais kwa asili mia 61 dhidi ya Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai aliyezoa asili mia 34 ya kura za Urais. Ijumaa wiki jana chama cha Tsvangirai cha MDC kiliondoa kesi mahakamani ya kupinga uchaguzi huo kikidai mahakama haiwezi kutekeleza haki.

MDC kilidai uchaguzi mkuu huo ulikumbwa na udanganyifu, madai yaliyopingwa na Muungano wa Ulaya na waangalizi wa kimataifa. Katika mkutano wa nchi za Kanda ya Kusini mwa Afrika, SADC ilisema kwamba Zimbabwe imefanya uchaguzi huru na haki na wakati umefika kwa vikwazo vya sasa kuondolewa.

Muungano wa Ulaya umesema uchaguzi wa Zimbabwe ulikua wa amani lakini kulikua na visa vya udanganyifu. Mugabe ametawala Zimbabwe tangu nchi hiyo kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka wa 1980.

Chanzo: bbc

Thursday, August 15

Misri: Waziri Mkuu atetea hatua ya polisi.


Waziri Mkuu wa muda wa Misri Hazem Beblawi ametetea oparesheni kali iliyochukuliwa ya kuvunja maandamano ambayo yamekuwa yakifanywa na wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani , Mohamed Morsi.
Bwana Beblawi amesema walilazimika kuchukua hatua hiyo kwani kulikuwa na haja ya kujeresha hali ya usalama na utulivu nchini humo.

Hata hivyo waziri huyo mkuu amesema haukuwa uamuzi rahisi kuwatawanya wafuasi hao wa Morsi.
Serikali ambayo imetangaza hali ya hatari nchini humo imesema wakati wa oparesheni hiyo idadi ya watu waliofariki dunia ni 235
Lakini Msemaji wa Muslim Brotherhood, wamesema idadi ya watu waliouwawa ni zaidi ya 2,000 huku maelfu ya wengine wakijeruhiwa.
"Idadi ya waliofariki dunia ni karibu elfu mbili, na maelfu ya wengine wamejeruhiwa au kupotea . Haya yamekuwa ,mauaji ya kinyama,umekuwa ni umwagikaji wa damnu , tumekuwa na uchaguzi huru, tukawa na rais aliyechaguliwa kwa njia huru, tukawa na katiba iliyopigiwa kura kwa njia huru na bunge la juu la nchi, hayo yote yamepuuzwa na kwa wakati huu watu wanapigwa risasi kiholela. Demkorasia iko kichinjioni nchini Misri", amesema Ahmed Moustapha ,msemaji wa Muslim Brotherhood mjini London.
Nao waandishi wa habari mjini Cairo wameripoti kuona maiti nyingi. Hata hivyo imekuwa vigumu kujua idadi kamili ya waliouwawa.
Kwa wakati huu polisi wamewakamata wakuu kadhaa wa Muslim Brotherhood na pia wamechukuwa udhibiti wa kambi mbili ambazo zimekuwa zikitumiwa na waandamanaji.
Katika taarifa yake kupitia televisheni, Bwana Beblawi ameeleza masikitiko yake kwa mauji yaliotokea na kutoa hakikisho kuwa sheria ya hali ya hatari itaondolewa haraka iwezekanavyo.
Waziri huyo mkuu pia amesema kuwa polisi walikuwa wamepewa amri ya kutotumia silaha wakati wa kuwatawanya waandamanji.
Amri hiyo ya hali ya hatari inayotazamiwa kuwepo kwa mwezi mzima katika mji wa Cairo na katika mikoa megine itakuwepo kuanzia jioni saa Moja hadi kumi na mbili saa za Misri.

BBC

Thursday, June 13

Uchaguzi kufanyika Julai 31 Zimbabwe

Mzozo wa kisiasa umeibuka nchini Zimbabwe baada ya rais Robert Mugabe kutoa agizo kuwa uchaguzi mkuu nchini humo utafanyika tarehe Thelathini na Moja Julai mwaka huu.
Waziri mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, ametoa taarifa muda mfupi tu baada ya agizo hilo la rais, akisema kuwa rais Mugabe amekiuka sheria kwa kutoshirikisha bunge na ameapa kupinga uamuzi huo.
Morganb Tsvangirai
Katika kikao na waandishi wa habari, Tsvangirai, amemshutumu Bwana Mugabe kwa kukiuka mkataba wa ugavi wa mamlaka uliosainiwa miaka mitano iliyopita, baada ya mzozo kuhusu matokeo ya kura kusababisha ghasia nchini humo.
Tsvangirai ametaka uchaguzi huo kuhairishwa hadi mageuzi ya kikatiba yafanyike ili kuhakikisha zoezi hilo la uchaguzi linafanyika kwa njia huru na haki.
Bunge la nchi hiyo bado linajadili mswada wa sheria ambao utaruhusu vyama vyote vya kisiasa kupewa nafasi sawa katika shirika la habari la serikali wakati wa kampeini.
Lakini wiki mbili zilizopita mahakama ya kikatiba nchini humo iliagiza kuwa uchaguzi huo ni sharti ufanyike kabla ya mwisho wa Julai.

BBC.

Tuesday, May 28

Sudan yatisha kufungia Sudan.K mafuta

Rais wa Sudan Omar al-Bashir ametishia, kufunga kabisa bomba la mafuta ambalo husafirisha mafuta kutoka Sudan Kusini hadi pwani ya Sudan, Red Sea.
Alisema kuwa Sudan itasitisha usafirishwaji wa mafuta ikiwa Sudan Kusini haitakoma kuwaunga mkono waasi wanaoendesha harakati zao katika eneo la mafuta la Sudan.
Licha ya Sudan Kusini kujitawala mwaka 2011, hali ya wasiwasi kuhusu mafuta na ardhi imekuwa ikiendelea.Jeshi la Sudan linapambana na waasi katika angalao maeneo matatu ya nchi hiyo.
''Na sasa natoa onyo la mwisho kwa ndugu zetu wa Sudan Kusini kuwa tutafunga kabisa bomba la mafuta ikiwa wataendelea kuunga mkono wasaliti katika jimbo la Darfur , Kordofan ya Kusini na Blue Nile'' alisema Bashir kupitia televisheni ya taifa huku akigusia waasi wanaoendesha harakati zao katika maeneo hayo.
Kundi la waasi lenye mirengo mingi, linalojulikana kama Sudan Revolutionary Front (SRF), limefanya mashambulizi katika miji kadhaa huku wakiteka mji mkubwa wa Um Rawaba , katikati mwa Sudan mwezi Aprili.
Kundi hilo linalonuia kuipindua serikali ya rais Bashir, lakini wakaendelea kudhibiti mji wa Abu Kershola, katika eneo jirani la Kordofan Kusini.
Waasi wa SPLM-North walijiunga na kundi la waasi la JEM kutoka Darfur pamoja na makundi mengine ambayo ni ya mrengo wa (SLA), kwa lengo la kubuni kundi la
Sudan Revolutionary Front mwaka jana.
Rais Bashir alitoa hotuba yake moja kwa moja kupitia televisheni ya taifa nchini Sudan, kufuatia tangazo la jeshi kuwa limeweza kuteka tena mji wa Abu Kershola kutoka kwa waasi.
Wakati huohuo, msemaji wa waasi hao aliambia shirika la habari la AFP kuwa wapiganaji waliondoka kutoka, eneo la Abu Kershola ili kulegeza vikwazo vya serikali kwa wenyeji wa eneo hilo.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukitetereka tangu mwaka 2011, wakati Sudan Kusini ilipoamua kujitawala.
Maswala muhimu kuhusu Uzalishaji wa mafuta, mizozo ya mipaka ynagali kutatuliwa.

BBC.

Wednesday, May 15

Rais wa Nigeria atangaza hali ya hatari

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ametangaza hali ya hatari katika majimbo matatu nchini humo, na kuamrisha wanajeshi zaidi wapelekwe katika majimbo hayo ili kukabiliana na kundi la Kiislamu la Boko Haram.
Kundi lenye msimamo mkali wa dini ya Kiislam la Boko Haram limezidisha mashambulizi dhidi ya vyombo vya usalama na shabaha za serikali katika ngome yake kaskazini-mashariki mwezi huu, hali iliyomlaazimu rais Jonathan kutangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa.

 "Baada ya mashauriano mapana, na kwa kutumia mamlaka niliyonayo chini ya vifungu vya ibara ya tatu, kifungu kidogo nambari moja cha katiba ya Nigeria ya mwaka 1999 kama ilivyofanyiwa marekebisho, natangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa," alisema rais Jonathan katika hotub yake iliyotangazwa moja kwa moja na vituo vya redio na televisheni.

Mgogoro wa viongozi wa kaskazini

Rais Jonathan pia alimuagiza mkuu wa majeshi nchini humo kupeleka vikosi zaidi katika majimbo hayo, katika hatua ambayo inaweza kumtumbukiza katika mgogoro na magavana wenye nguvu na viongozi wa kaskazini, ambao tayari ana uhusiano wa mashaka nao. Siku ya Jumatatu, jukwa la magavana wa Nigeria, ambalo linawakilisha magavana wa majimbo 36 ya nchi hiyo walimuonya Jonathan dhidi ya kuweka utawala wa hatari kama jawabu kwa uasi wa Boko Haram.
Maagizo yake yanafuatia ushahidi unaoongezeka kuwa kundi la Boko Haram sasa linadhibiti maeneo kaskazini-mashariki, karibu na ziwa Chad, ambako maafisa wa serikali wameripotiwa kukimbia. Duru za usalama zinasema kundi hilo linadhibiti angalau maeneo 10 ya utawala katika jimbo la Borno, ambalo ndiyo kitovu cha uasi wake.


Boko Haram yadhibiti maeneo kaskazini

Wapiganaji kadhaa wa kundi hilo wakiwa katika mabasi na magari yaliyofungiwa bunduki za rasharasha yaliuzingira mji wa Bama jimboni Borno wiki iliyopita, na kuwaachia wafungwa zaidi ya 100, na kuua watu 55 wengi wao wakiwa maafisa wa polisi na wanajeshi.
Na siku kadhaa kabla, watu kadhaa waliuawa katika kijiji cha uvuvi cha Baga ambacho pia kiko jimboni Borno karibu na ziwa Chad, wakati kijiji hicho kilipovamiwa na vikosi vya Nigeria, Niger na Chad vikiwasaka wapiganaji wa Boko Haram. Wenyeji wa kijiji hicho walisema wanajeshi hao walihusika na mauaji makubwa ya raia.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau alisema katika mkanda wa video wiki hii kuwa kundi lake limewateka wanawake na watoto wengi katika ulipizaji dhidi ya vikosi vya usalama, ambavyo alisema vinawashikilia wake na watoto wa wanachama wa kundi hilo pasipo na kosa lolote. Shekau pia alikataa pendekezo la rais Jonathan la kutoa msamaha kwa wapiganaji wa kundi, hali ambayo yumkini imechochea amri hii ya hali ya hatari.

Kumekuwepo na ongezeko la vurugu katika majimbo mengine ya Nigeria, ambapo maafisa 46 wa polisi waliuawa na watu wenye silaha katika shambulio la kuvizia katika jimbo la kati la Nassarawa wiki iliyopita, ambapo maafisa walililaum kundi la madhehebu ambalo halihusiki na Boko haramu.

DW - SWAHILI.

Tuesday, May 14

Obama, Cameron wamshinikiza Putin kuhusu Syria

Marekani na Uingereza zimeongeza shinikizo kwa Urusi juu ya mgogoro wa Syria, lakini rais Barack Obama ameonya kuwa hakutakuwa na suluhisho la haraka la mgogoro huo, huku jeshi la Assad likipata mafanikio zaidi.
Obama na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron walitaka kujenga hamasa mpya nyuma ya mkutano wa kimataifa wa Syria unaodhaminiwa na Marekani na Urusi, ambao sasa unatarajiwa kufanyika mwezi Juni, wakati wawili hao walipokutana mjini Washington.
Cameron, akiwa ndiyo amekamilisha ziara nchinin Urusi, alisema anaamini London, Washington na Moscow wamepata muafaka juu ya mgogoro wa Syria, ambao umegharimu maisha ya maelfu ya watu. Obama alisema Urusi ina maslahi na wajibu wa kusaidia kukomesha mgogoro huo, akisema alikuwa amewasilisha ujumbe kwa rais Vladmir Putin kabla ya ziara ya waziri wake wa mambo ya kigeni mjini Moscow wiki iliyopita.

Hali bado ni ngumu sana Syria

Lakini, Obama alionya kuwa itakuwa vigumu sana kuishawishi Urusi kubadilisha msimamo wake, na kubainisha kuwa bado kuna tofauti za msingi kati ya nchi hiyo na mataifa ya magharibi. Obama alisema hata kama Urusi itashawishika na kusimama upande wao, hali nchini Syria bado ni ngumu sana kutokana na ushiriki wa Iran, kundi la Hezbollah na wapiganaji walio na mafungamano na mtandao wa Al-qaeda katika mgogoro huo.
"Siahidi kuwa kutakuwepo na mafanikio. Ukweli ni kwamba miungu ya ghadhabu ikishaachiwa katika hali kama tunayoshuhudia nchini Syria, inakuwa vigumu sana kuweka tena mambo sawa," alisema Obama.

Cameron aonyesha matumaini

Kwa upande wake, waziri mkuu Cameron alikuwa mwenye matumaini zaidi, akisema anaamini London, Washington na Moscow zimefikia muafaka juu ya mgogoro huo. Cameron alisema kuwa historia ya Syria inaandikwa kwa kutumia damu ya raia wa nchi hiyo, huku dunia ikitizama tu, na kuongeza kuwa wakati umefika kwa dunia kuja pamoja na kukomesha umuagaji huu wa damu. Cameron pia aliahidi kuongeza msaada usio wa kijeshi kwa baadhi ya makundi ya waasi nchini Syria kwa mara mbili katika kipindi cha mwaka ujao.
"Kama hatuusaidii upinzani nchini Syria ambao tunautambua kuwa halali, na uliosaini tamko kuhusu mustakabali wa Syria yenye kidemokrasia, inayoheshimu haki za wachache, tusipofanya kazi na upande huo, basi tusishangae kuona makundi yenye itikadi kali yakizidi kuongezeka," alisema Cameron.

Hezbollah yaupiga tafu utawala wa Assad

Cameron na Obama walikutana huku kukiwa na ishara kuwa utawala wa Assad hautanguka kwa urahisi, wakati jeshi lake likipata mafanikio dhidi ya waasi katika mkoa muhimu wa Homs, kwa msaada wa kundi la Hezbollah, kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria.
Katika mkoa wa kusini wa Daraa, ambao ndiyo chimbuko la uasi dhidi ya Assad, jeshi la serikali lilichukua udhibiti wa mji wa Khirbet Ghazaleh, uliyoko katika njia kati ya Damascus na mpaka wa Jordan. Shirika hilo lilisema siku ya Jumatatu kuwa limeorodhesha vifo vya watu wapatao 82,257 tangu kuanza kwa vita hivyo Machi 2011, wakiwemo raia wa kawaida 34,473.
Katika ishara nyingine ya kuongezeka kwa juhudi za kidiplomasia, Ikulu ya kremlin imesema kuwa waziri mkuu wa Israel Benjanim Netanyahu atafanya mazungumzo na rais Putin leo, kujaribu kuishawishi nchi hiyo iachane na mpango wake wa kunedelea kuiuzia Syria silaha. Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon naye ataizuru Urusi siku ya Ijumaa, wakati waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akitarajiwa kuwa na mazungumzo na raias Obama mjini Washington leo.

Serikali, waasi bado kuthibitisha ushiriki wao

Mkutano wa Syria unaoandaliwa na Marekani na Urusi unatarajiwa kufanyika mwezi Juni, lakini taarifa za maandalizi yake bado hazijawekwa bayana. Wapinzani wamesema  watashauriana na wafadhili wao - nchi za Saudi Arabia, Qatar na Uturuki kabla ya kuamua kushiriki katika mazungumzo hayo, huku Syria nayo ikisema inataka ipewe maelezi kamili juu ya mkutano huo kabla ya kuamua kuhusu ushiriki wake.
Waziri wa mawasiliano Omran Zoabi, amesema Syria inakaribisha pendekezo hilo, lakini akasisitiza kuwa nchi yake haitakuwa sehemu ya mkutano unaoumiza uhuru wa Syria kwa njia yoyote ile. Zoabi aliongeza kuwa uamuzi juu ya jukumu la rais Bashar al-Assad uko mikononi mwa raia wa Syria tu kupitia sanduku la kupigia kura.

DW - SWAHILI.

Mgomo wazuka mgodini Afrika Kusini

Kampuni ya uchimbaji madini ya Lonmin, nchini Afrika Kusini inasema kuwa maelfu ya wafanyakazi katika mgodi wake wa wa platinum wamefanya mgomo kinyume cha sheria baada ya afisa wa muungano wao kupigwa risasi katika baa moja mwishioni mwa juma.
Msemaji wa kampuni hiyo Sue Vey amesema kuwa shughuli zote za uzalishaji kwenye kiwanda hicho zimevurugika .
Mgomo huu umezua hofu ya vurugu zaidi kutokea baada ya sekta hiyo kukumbwa na migomo mwaka jana
Mwezi Agosti mwaka jana wafanyakazi thelathini na wanne waliuliwa na polisi katika mgodi wa Marikana na waandishi wa habari wanasema mgomo huo umesababisha hofu ya kutokea kwa ghasia kufuatia hali ya taharuki iliyopo juu ya kukatwa kwa kazi , mashauriano ya riba na uhasama ndani ya muungano wa wafanyakazi.
Lonmin, ambayo hisa zake,ziko katika soko la hisa la London na Johannesburg , ndiyo kampuni ya tatu kwa ukubwa katika kuzalisha madini ya platinum.
Taarifa za mgomo wa leo zimesababisha hisa za kampuni hiyo kushuka kwa asilimia 5% mjini London.
Msemaji wa kampuni hiyo, Sue Vey alisema kuwa migodi yote kumi na mitatu ya kampuni hiyo imefungwa kwa sasa.
"Wafanyakazi wa kampuni hiyo waliwasili kazini ingawa hawakuelekea katika shughuli zao kama ilivyo desturi yao
Huku akisema kuwa kampuni hiyo haielewi kwa nini wafanyakazi wameamua kugoma, msemaji wa chama cha wafanyakazi hao, alisema kuwa huenda mgomo huo unatokana na ghadhabu ya wafanyakazi hao, kuhusu mauaji yaliyotokea mwishoni mwa wiki ya kiongozi mmoja wa chama hasimu cha wafanyakazi.
Polisi walithibitisha kuwa kiongozi huyo aliuawa mwishini mwa wiki katika eneo Rustenburg.

BBC - SWAHILI.

Sunday, May 12

Nawaz Sharif kurejea madarakani; Pakistan

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif anaendelea kuongoza katika uchaguzi wa bunge nchini Pakistan, kwa mujibu wa matokeo ya awali leo
Sharif aliangushwa   kutoka  madarakani  katika  mapinduzi  mwaka 1999, akafungwa  na  kupelekwa  kuishi  uhamishoni. Nawaz ameweza  kurejea  tena  kwa  kishindo  na  kupata  ushindi  katika uchaguzi  na leo  Jumapili (12.05.2013) anaelekea  kupata uongozi kwa  kipindi cha  tatu  katika  uchaguzi  mkuu  kama  waziri  mkuu  wa Pakistan.
Kituo  cha  binafsi  cha  televisheni cha Geo  kimeripoti  kuwa chama  cha  Nawaz  cha  Pakistan Muslim League-Nawaz (PML-N) kinaongoza  katika  majimbo 126  ya  ubunge  kati  ya  majimbo  268 yanayowaniwa.
Kituo  cha  televisheni  cha Dunya  kimesema  kuwa  chama  cha PML-N tayari  kimepata  viti  80. Kituo  cha  taifa  cha  televisheni nchini  Pakistan  pia kimesema  chama  hicho  kinaongoza.
Matokeo  ambayo  si  rasmi yanaonesha   kuwa  chama  cha Pakistan Tehreek-e-Insaf cha  mchezaji  wa  zamani  nyota  wa mchezo  wa  kriketi   Imran Khan kiko  katika  nafasi  ya  pili.
Chama  tawala  cha  zamani  cha  Pakistan Peoples  Party  cha  rais Asif Ali  Zardari  kinafuatia.

Vyama vya kidini havikufua dafu

Vyama  vya  kidini  vyenye  mtazamo  wa   mrengo  wa  kulia vimeshindwa  kupata  mafanikio  ya  maana.
Maafisa  wa  uchaguzi  wamesema  kuwa  watu  waliojitokeza kupiga  kura  walikuwa  ni  kiasi  ya  asilimia 60  ya  wapiga  kura milioni 86  wenye  haki  ya  kupiga  kura , ikiwa  ni idadi  kubwa kuwahi  kujitokeza  kupiga  kura. Asilimia  44  tu  ya  wapiga  kura walijitokeza  katika  uchaguzi  mkuu  mwaka  2008.

Uchaguzi  wa  kihistoria

Uchaguzi  huo ni  wa  kwanza  katika  historia  ya  nchi  hiyo , ambapo  kunafanyika  mabadiliko  kwa  njia  ya  kidemokrasia kutoka  utawala  mmoja  wa  kiraia  kwenda  kwenda  kwa  mwingine.
Mkuu  wa  tume  ya  uchaguzi  Fakhruddin Ibrahim amejiita  "mtu mwenye  furaha", baada  ya  kutangaza  kuwa  uchaguzi  huo umefanyika  kwa  uwazi.
"Sasa mpira  uko  upande  wenu, mtaamua  kupata  serikali  yenye utawala  mzuri," jaji  huyo  mstaafu  ameuambia  mkutano  na waandishi  wa  habari  mjini  Islamabad.

Ghasia

Ghasia  za  siku  ya  uchaguzi  hata  hivyo  zimesababisha  vifo  vya watu  28  na  wengine  91  wamejeruhiwa  katika  mashambulio  ya mabomu  pamoja  na  mashambulio yaliyolenga  maeneo  maalum.
Kwa  jumla  viti  272  vinagombaniwa   katika  bunge  la  taifa , baraza  la  wawakilishi  ambalo  lina jukumu  la  kuunda  serikali. Katika  majimbo  manne  ya  uchaguzi , uchaguzi  umefutwa kutokana  na  sababu za  kiusalama.
Uchaguzi  huo  pia  unajumuisha  viti 577  katika  mabunge  manne ya  majimbo.

DW - SWAHILI.

Friday, May 10

Merkel ziarani Afghanistan

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Ijumaa(10.05.2011)amefanya ziara ya ghafla kaskazini mwa Afghanistan kuvitembelea vikosi vya nchi yake siku sita baada ya kuuwawa kwa mwanajeshi wa kikosi maalum cha Ujerumani.
Msemaji wa kijeshi Luteni Kanali Marco Schmidt amesema Kansela Angela Merkel amewasili katika mji wa Mazar-e-Sharif wakati wa asubuhi leo hii ambapo alikuwa akitegemewa kuwepo kwa masaa machache tu. Msemaji huyo kwa sababu za kiusalama amekataa kutowa maelezo zaidi ila amesema kwamba hakuna mipango kwa Merkel kukutana na Rais Hamid Karzai au kuzungumza na rais huyo wa Afghanistan kwa njia ya simu.Katika ziara yake hiyo Merkel ameandamana na Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere.
Hapo tarehe 4 mwezi wa Mei waasi waliokuwa wakivurumisha maroketi wamemuuwa mwanajeshi mmoja wa Ujerumani na kumjeruhi mwengine katika jimbo la kaskazini la Baghlan. Hiyo ni mara ya kwanza kutokea kwa kifo cha mwanajeshi wa kikosi maalum cha Ujerumani kilioko Afghanistan.Kikosi hicho kinahesabiwa kuwa na ujuzi mkubwa ni kama kile cha Marekani kinachojulikana kwa jina la Navy SEAL ambapo wakati huo kilikuwa kikiongoza operesheni za kijeshi nchini Afghanistan.Wanajeshi wa Ujerumani 35 wameuwawa nchini Afghanistan tokea mwaka 2002. Ujerumani ina vikosi vingiIkiwa na zaidi ya wanajeshi 4,000 waliowekwa nchini Afghanistan Ujerumani ni nchi ya tatu yenye wanajeshi wengi katika kikosi cha kimataifa kilioko Afghanistan na imeahidi kubakisha wanajeshi 800 nchini humo baada ya operesheni ya mapambano ya NATO kumalizika mwishoni mwa mwaka 2014.
Marekani inatarajiwa kubakisha wanajeshi 10,000 nchini Afghanistan baada ya mwaka 2014 lakini bado haukufikiwa uamuzi rasmi juu ya suala hilo.
Vikosi vya Ujerumani vitaendelea kubakia hadi hapo mwaka 2017 kwa ajili ya kutowa mafunzo,ushauri na msaada kwa vikosi vya usalama vya Afghanistan na vitawekwa katika mji mkuu wa Kabul na Mazar-e-Sharif. Baada ya mwaka 2017 Ujerumani imesema itakuwa tayari kuchangia wanajeshi 200 hadi 300.
Sharti la kubakisha vikosi
Uamuzi wa mwisho kuhusu vikosi vya Ujerumani vitakavowekwa nchini Afghanistan baada ya mwaka 2014 utatolewa na serikali mpya baada ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika hapo mwezi wa Septemba ambapo kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni Merkel anatarajiwa kushinda muhula wa tatu wa kipindi cha miaka mingine minne madarakani. Wakati mpango huo wa kuwekwa kwa vikosi vya Ujerumani nchini Afghanistan kwa kiasi kikubwa haungwi mkono na wananchi, unaungwa mkono na vyama vikuu vya kisiasa.
Suala la Ujerumani kuendelea kuweka vikosi vyake nchini Afghanistan pia linahitaji ombi la serikali ya nchi hiyo.Katika hafla iliofanyika katika mji mkuu wa Kabul hapo Alhamisi,Rais Hamid Karzai amesema alikuwa anataka kila nchi mwanachama wa nchi 28 za Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuzungumza moja kwa moja na serikali yake juu ya idadi ya wanajeshi inaotaka kuwaweka nchini humo,mahala pa kuwaweka na vipi vikosi hivyo vitakvyoweza kuinufaisha nchi hiyo.

Thursday, May 9

Wapiganaji wa al-Shabaab wanaomtii Godane waripotiwa kumuua al-Amriki

Mpiganaji wa jihadi aliyezaliwa Marekani, Omar Hammami, anayefahamika pia kama Abu Mansour al-Amriki, aliripotiwa kuuawa na wanajeshi wa al-Shabaab wanaomtii kamanda wa juu wa kundi hilo, Ahmed Abdi Godane, jioni ya Jumanne (tarehe 7 Mei) karibu na kijiji cha Rama Addey kusini mwa Somalia, iliripoti Radio Bar-Kulan inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa.Kwa mujibu wa taarifa ambazo bado hazijathibitishwa, kiongozi wa ngazi ya juu wa al-Shabaab, Fuad Mohamed Qalaf, anayejulikana kama Fuad Shangole, alitoa tangazo hilo jioni ya Jumanne katika hotuba ya jioni baada ya magharibi katika msikiti mmoja wa Bulo Burde mkoani Hiran. Alisema kwamba al-Amriki alivamiwa na mapigano ya risasi yalizuka na kusababisha wanamgambo kadhaa wa al-Shabaab kuuawa.
Katika hotuba yake, Shangole alisema watu waliomuua al-Amriki wametenda kinyume na misingi ya Uislamu, hoja ambayo hapo nyuma ilisemwa na viongozi kadhaa wa juu wa al-Shabaab -- wakiwemo mmoja wa waasisi Ibrahim al-Afghani, kiongozi wa wapiganaji wa kigeni al-Zubayr al-Muhajir na Sheikh Mukhtar Robow Ali (au Abu Mansur) - katika fatwa ya tarehe 30 Aprili iliyokataza kumuua al-Amriki.
Al-Amriki aliwekwa kwenye orodha ya Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) ya magaidi wanaosakwa sana mwezi Novemba na mwezi Machi Marekani ikatangaza zawadi ya dola milioni 5 kwa kichwa chake.
Al-Amriki aliaminika kujificha nchini Somalia na mara kwa mara aliwasiliana na wafuasi wake na wachambuzi wa kimataifa wa masuala ya ugaidi kupitia Twittter katika miezi ya karibuni. Taarifa yake ya mwisho kwenye Twitter ilikuwa ni tarehe 3 Mei baada ya kutuma picha na taarifa kadhaa akiwashutumu wapiganaji wa al-Shabaab wanaomtii Godane kwa kujaribu kumuua.
Katika kipindi cha wiki moja tangu kushindwa kwa jaribio hilo la mauaji, al-Amriki alionekana kuwa na hali ya hatari, akituma taarifa zisizo na shaka juu ya hatari aliyoamini kuwa inamkabili.
"Labda sitaweza kupata tena nafasi ya kutuma taarifa kwenye Twitter lakini kumbuka tu tuliyosema na tuliyoyaamini. Mungu aliniweka hai ili nifikishe ujumbe kwa umma," aliandika hapo tarehe 29 Aprili.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, al-Amriki alituma vidio, nyaraka na taarifa kwenye mitandao ya Twitter na YouTube zinazoeleza kwa undani namna ambavyo uongozi wa al-Shabaab - hasa Godane, anayefahamika pia kama Abu Zubayr -- umekuwa sababu ya kuporomoka kwa kikundi hicho, na jinsi uongozi wa Godane ulivyo kinyume na misingi ya kweli ya jihadi.
Hata kwenye taarifa zake za mwisho kwenye Twitter, al-Amriki aliendeleza mashambulizi yake dhidi ya Godane. "Abu Zubayr ameingiwa na wazimu. Anaanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe," aliandika al-Amriki tarehe 26 Aprili.
Kifo cha al-Amriki hakikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru, na hii si mara ya kwanza kwa habari kama hiyo kusambazwa. Mwezi Aprili 2012, vyombo vya Somalia viliripoti kwamba al-Shabaab ilimuua al-Amriki, ambapo baadaye iligundulika kuwa ni makosa.
SABAHI ONLINE.

Roberto Avezedo ndiye kiongozi mpya wa WTO

Umoja wa Ulaya, Marekani na China ni miongoni mwa nchi ambazo zimesema zitamuunga mkono mkuu mpya wa Shirika la Biashara Duniani – WTO, Mbrazil Roberto Avezedo.
 alimshinda mgombea mwenzake Herminio Blanco wa Mexico ambaye alikuwa akipigiwa upatu na Marekani pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya katika duru ya mwisho ya kinyan'ganyiro hicho kuchukuwa nafasi ya Pascal Lamy ambaye anan'gatuka hapo mwezi wa Augosti. Roberto Avezedo mwenye umri wa miaka 55 na ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Brazil katika Shirika la Biashara Duniani – WTO, alipata uungwaji mkono mkubwa kutoka nchi zinazoinukia kiuchumi duniani.
Kaimu mwakilishi wa Marekani kuhusu biashara Demetrios Marantis amesema Marekani imefurahishwa na uamuzi wa pamoja wa kumteuwa Roberto Azevedo kama Mkurugenzi mkuu wa WTO, na inatazamia kufanya kazi naye na wanachama wengine katika kulifanya shirika hilo kuwa imara, na lenye mafanikio katika siku zijazo.Naye Kamisha wa Biashara katika Umoja wa Ulaya Karel De Gucht amesema anaamini Azavedo atasaidia kuyafufua mazungumzo ya kibiashara yaliyokwama ya Doha, wakati wa mkutano wa mawaziri wa WTO mjini Bali mwezi Desemba. Mazungumzo ya Doha ambayo yalianzishwa katika mkutano wa kilele nchini Qatar mwaka wa 2001, yanalenga kufikia muafaka kuhusu kufungua biashara na kuondoa vizingiti vya kibiashara kama vile ruzuku, kodi nyingi kupindukia, na kanuni za kushirikisha biashara ya kimataifa kuzisaidia nchi maskini. Azevedo amezitaka nchi zinazolumbana kuitathmini misimamo yao kwa sababu shirika la WTO lina umuhimu katika maisha ya kila mwananchi kote ulimwenguni, iwe wanalifahamu hilo au la. Ujumbe mwingine umetolewa na Canada ambayo imemtaka kiongozi huyo mpya kukabiliana na kitisho kinachosababishwa na ulinzi wa masoko katika juhudi za kuufufa uchumi wa ulimwengu.
China imeukaribisha uteuzi huo ikisema umedhihirisha mshikimanano mkubwa wa nchi nchi zinazoinukia kiuchumi. Shirika la Habari la China limesema uteuzi wa Azevedo ni kitu cha kujivunia kwa sababu ndio mara ya kwanza kwa mgombea kutoka kundi la nchi zinazoinukia kiviwanda BRICS- yaani Brazil, China, India, Urusi na Afrika Kusini, amepewa wadhifa huo.
Akizungumzia uteuzi wake, Azevedo amewashukuru wagombea wenzake wanane walioshiriki katika kinyang'anyiro hicho, akisema kuwa kiwango chao cha ujuzi na utaalamu kilimanaanisha kuwa pangekuwa na Mkurugenzi Mkuu mpya mwenye ubora wa hali ya juu, bila kuzingatia yule angechaguliwa.
Katika taarifa, rais wa Brazil, Dilma Roussef amesema chaguo la Azevedo ni ushindi kwa shirika zima la WTO. WTO humchagua kiongozi wake kwa misingi ya maelewano na wala siyo kupitia uchaguzi. Shirika la Biashara Duniani limesema Azevedo ataidhinishwa rasmi na nchi wanachama mnamo Mei 14 na kisha kuchukua rasmi wadhfa huo mnamo Septemba mosi.

DW - KISWAHILI.

Marekani yasema Assad asiwe katika serikali ya mpito

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema rais wa Syria Bashar al-Assad atapaswa kuondoka madarakani, kama sharti la mpango wowote wa kuusuluhisha mgogoro wa Syria kupitia njia za kisiasa.
Akizungumza mjini Roma baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Jordan Nasser Judeh, John Kerry amesema kuwa wadau wote katika juhudi za kutafuta amani nchini Syria, wanashughulikia kuundwa kwa serikali ya mpito itakayokubaliwa na pande zinazohasimiana nchini humo. Hata hivyo, waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amesisitiza kuwa kwa maoni yao, rais Bashar al-Assad hapaswi kuhusika katika serikali hiyo. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekubaliana na maoni hayo ya John Kerry.
''Sisi pia maoni yetu ni kwamba Bashar al-Assad amepoteza uhalali wa kuwa kiongozi. Lakini pia tunafahamu kuwa tunalo jukumu la kuweka mchakato utakaowezesha kufanikisha kipindi chote cha mpito.'' Amesema kansela Merkel.
Muafaka wa kimataifa
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry katika mazungumzo na viongozi wa Urusi mjini Moscow
Kerry pia alisema mchakato wa kufanyika kwa mkutano wa kimataifa kuhusu Syria ulikuwa ukiendelea, baada ya kukubaliana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kwamba nchi zao zitashirikiana katika suala hilo. Alisema alizungumza na mawaziri wa nchi za nje wa mataifa yote yanayohusika katika mkutano huo, na kuongeza kuwa mawaziri wote hao waliukaribisha mkutano huo, na kuelezea utashi wao kushiriki katika juhudi zote za kumalizia vita vya Syria kwa njia ya mazungumzo.
Aidha, John Kerry alisema amewasiliana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, na kuongeza kuwa pande zote zinazohusika zitafanya hima kuuandaa mkutano huo. Mkutano huo wa kimataifa kuhusu Syria unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, ingawa mahali utakapofanyika bado hapajaamuliwa.
Katika juhudi hizo hizo za kutafuta suluhu kwa mzozo wa Syria, Rais wa Marekani Barack Obama atakutana na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron mjini Washington Jumatatu ijayo, kuzungumzia suala hilo. Viongozi hao pia watakutana tena kwenye mkutano wa nchi nane zinazoongoza kiviwanda, utakaofanyika mwezi ujao huko Ireland ya Kaskazini.
Kabla ya kwenda Marekani, Cameron atafanya mazungumzo na rais wa Urusi Vladimir Putin Ijumaa wiki hii. Cameron amesema mazungumzo yake na Putin yatahusu kile alichokiita ''hatua za dharura'' kuelekea kipindi cha mpito kitakachomaliza umwagaji damu nchini Syria.
Al-Nusra yakanusha
Makundi ya waasi wa Syria yamekuwa yakishukiwa kushirikisha wenye msimamo mkali wa kiislamu
Nchini Syria kwenyewe, kundi lenye nguvu la al-Nusra lenye msimamo mkali wa kiislamu, limekanusha taarifa kuwa kiongozi wake Abu Mohammed al-Jawlani amejeruhiwa kwenye uwanja wa mapambano karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus. Kamanda wa kundi hilo al-Ghareeb al-Muhajir al-Qahtani amesema kuwa taarifa hizo zilizotangazwa na vyombo vya habari ni uongo wa serikali ya rais Bashar al-Assad.
Kujeruhiwa kwake pia kulitangazwa na shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, ambalo lilisema kuwa alipata jeraha mguuni.
Kundi la al-Nusra, mwezi uliopita lilitangaza utiifu wake kwa kiongozi wa mtandao wa al-Qaida Ayman al-Zawahri, na kuthibitisha kile ambacho kilikuwa kikishukiwa kuwa baadhi ya makundi ya waasi wa Syria yalikuwa na mafungamano na mitandao ya kigaidi.

Rais Joachim Gauck ziarani Amerika Kusini

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck leo (09.05.2013) anaanza ziara ya siku tisa katika bara la Amerika Kusini, ambayo itampeleka kwanza Colombia na baadae Brazil, mshirika muhimu zaidi wa Ujerumani Amerika ya Kusini.
Akiwa nchini Brazil, ambayo ndiyo taifa la sita kwa uchumi mkubwa duniani, Gauck anatarajiwa kujikita katika masuala ya kiuchumi, na nchini Colombia atazungumzia haja ya maridhiano ya kitaifa. Serikali ya Colombia kwa sasa inashiriki mazungumzo na kundi la waasi wa "Revolutionery Armed Forces of Colombia" FARC, mchakato ambao kwa mara ya kwanza umeonyesha matumaini ya kufanikiwa. Mgororo wa nchi hiyo uliodumu kwa nusu karne sasa, umegharimu maisha ya watu karibu laki mbili, na kusababisha wengine milioni 4 kuyakimbia makaazi yao.
Rais wa Colombia, Juan Manuel Santos.
Gauck ambae ni mchungaji wa zamani wa kilutheri na mwanaharakati wa kupinga ukomunisti kutoka Ujerumani ya Mashariki, ana uzoefu mkubwa katika mchakato wa ushirikishwaji na anatarajiwa kuzungumzia suala hilo mara nyingi wakati wa ziara yake. Ujerumani inajiona kama mshirika katika mdahalo wa Colombia, na imekuwa ikielekeza msaada wake kwa uendelezaji wa mchakato wa amani. Ingawa hali ya haki za binaadamu nchini humo haiwezi kuchukuliwa kama isiyo na matatizo, serikali ya rais wa Colombia Juan Manuel Santos inachukuliwa kuwa katika njia sahihi kwa mujibu wa ofisi ya rais wa Ujerumani.
Maridhiano miongoni mwa jamii ya Wacolombia ni sharti la kupatikana kwa mafanikio ya kiuchumi. Serikali ya Ujerumani imeikubali Colombia kuwa miongoni mwa shabaha zake za masoko, na nchi hiyo ndiyo mshirika mkuu wa Kibishara wa Colombia katika bara la Ulaya, na kimataifa, ujerumani ni nchi ya nne nyuma ya Marekani, China na Mexico.
Uchumi kuzungumzwa Brazil
Rais Gauck ataizuru Brazil siku ya Jumapili, ambapo masuala ya kiuchumi ndiyo yatakuwa kwenye ajenda yake. Ziara yake mjini Sao Paulo itaashiria kuanza kwa mwaka wa Ujerumani katika taifa hilo la Amerika Kusini, ambao mtangulizi wa Gauck Chritian Wulff alikubaliana na Rais wa Brazil Dilma Rousseff kuuanzisha mei 2011.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameizuru Brazil mara moja tu katika uongozi wake, mwaka 2008. Mwaka uliyopita, alifuta ushiriki wake katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu, maarufu kama Rio+20, jambo lililowasikitisha Wabrazil. Jumuiya ya wafanyabiashra wa Ujerumani nchini Brazil wangependa kumuona Merkel tena, kwa sababu nchi hiyo ndiyo mshirika imara zaidi wa kiuchumi wa Ujerumani katika Amerika ya Kusini, na Gauck anatizamiwa kusafisha njia kwa ajili ya ziara hiyo.
Rais wa Brazil, Dilma Rousseff.
Gauck anaongoza ujumbe mkubwa wa kiuchumi, unaojumlisha wataalamu wa mazingira na teknolojia ya dawa, uhandisi, usafiri wa anga na usafirishaji, pamoja na wawakilishi wa sekta ya ujenzi na usanifu majengo. Wafanyabiashara wa Ujerumani wanatumaini kushiriki katika miradi ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mashindano ya kombe la dunia mwaka 2014, na michezo ya olimpiki mwaka 2016 na pia katika upanuzi wa bandari za nchi hiyo.
Kuna karibu makampuni 800 ya Ujerumani yanayoendesha shughuli zake katika mji wa Sao Paulo peke yake. Mji huo unaoshikilia uchumi wa Brazil ndiyo unaochukuliwa kuwa na shughuli nyingi za viwanda vya Kijerumani nje ya Ujerumani. Lakini uchumi wa nchi hiyo ulipungua kasi na kufikia kiwango cha ukuaji cha asilimia 0.9 tu mwaka uliyopita, huku mfumuko wa bei ukiwa asilimia 5.8, na unatarajiwa kuendelea kuwa katika kiwango hicho mwaka huu.

Wednesday, May 8

Waasi wa PKK waanza kuondoka Uturuki

Wapiganaji waasi wa Kikurdi wameanza kuondoka kusini mashariki mwa Uturuki kwenda kwenye ngome zao nchini Iraq chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, kimeeleza chanzo cha habari cha Wakurdi.

"Tunafahamu kwamba, wameanza kuondoka," Selahattin Demirtas, mwanasiasa wa Kikurdi aliyeshiriki katika mchakato wa amani ameliambia shirika la habari la AFP.

Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi (PKK) kilitangaza mwezi uliopita kwamba, wapiganaji hao wataondoka kwa awamu kuanza mapema Mei .

Zaidi ya watu 40,000 wameuawa katika mapigano ya miaka 30 ya kuipinga Uturuki.

Gultan Kisinak, ambaye ni naibu kiongozi wa Chama cha Amani na Demokrasia (BDP) pamoja na Bwana Demirtas waeliambai shirika la habari la Associated Press kwamba, kundi la kwanza la wapiganaji limeanza kuelekea upande wa kaskazini mpakani na Iraq.

Inaaminika kwamba, chama cha PKK kinawapiganaji wanaofikia 2,000 ndani ya Uturuki na itawachukua muda wa miezi minne kwa wote kuondoka kabisa nchini humo.

Wanatarajiwa kuvuka mpaka kwa miguu na kuelekea kwenye ngome zao katika milima ya Qandil nchini Iraq.

Abdullah Ocalan kiongozi mkongwe wa PKK aliyeko gerezani nchini Uturuki, aliamuru kuondoka kwa wapiganaji wake mwezi Machi kama sehemu ya majadiliano ya amani na serikali ya Ankara.

Msemaji wa PKK, Bakhtiyar Dogan, ameliambia gazeti la Uturuki la Hawlati kwamba, kati ya wapiganaji 200 hadi 500 wataondoka siku ya Jumatano.

Amesema wapiganaji hao wataondoka kutoka maeneo ya Semdinli na Sirnak ya Uturuki wakiwa katika makundi matatu.

Kwa mujibu wa AFP, wapiganaji wa PKK walilalamika kuwa katika kilele cha siku ya kuondoka kwao, Uturuki iliongeza idadi ya wanajeshi wake eneo la mpakani na ilikua ikirusha ndege za doria.
Wamedai kuwa vitendo kama hivyo vinachelewesha mchakato wa amani na kuchochea uchokozi na mapigano.

Hata hivyo jeshi la Uturuki halijathibitisha iwapo hatua za ziada zimechukuliwa lakini limesema mapambano yake dhidi ya ugaidi yanaendelea.

Kaimu kiongozi wa PKK, Murat Karayilan, Aprili mwaka huu alionya kuwa wapiganaji wake watajibu na shughuli ya kuondoka ingesitishwa endapo wangeshabuliwa.

Wakati wa kuondoka mwaka 1999, jeshi la Uturuki liliwashambulia waasi hao na kuwaua wapiganaji wake 500.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, mara kadhaa ameahidi kuwa, jeshi halitamshambulia mpiganaji yeyote wa PKK atakayekuwa anaondoka.

Siku ya Jumanne, Bw. Erdogan alisema kuwa, kuweka silahachini ndio kiwe kipaumbele cha kwanza ili mchakato wa amani uweze kufanikiwa.

Nigeria:watu 55 wauawa katika shambulio

Taarifa zinasema, wafungwa 105 walitoroshwa katika shambulio hilo mapema alfajiri lililotokea katika jimbo la Bama, Borno.
Aidha, mashahidi na jeshi linasema kituo cha polisi cha Bama, majengo ya serikali na kambi za kijeshi ziliteketezwa kwa moto.
Habari zinasema, mashambulio ya makundi yenye msimamo mkali ni ya kawaida katika jimbo hilo lakini kiwango cha umwagaji damu kilichotokea katika shambulio la sasa ni cha kutisha.
Mwandishi wa BBC jijini Lagos, Will Ross, anasema shambulio hilo linafuatia mashambulio mengine mabaya siku za nyuma linakinzana na taarifa kwamba, operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo hao zimepunguza tishio la Boko Haram.
Rais Goodluck Jonathan ameunda kamati itakayopitia masharti ya msamaha kwa waasi hao lakini kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, mpaka sasa amekataa wazo hilo.
Msemaji wa jeshi, Musa Sagir, aliyeko mji wa Maiduguri takriban kilomita 70 kutoka Bama, amedai kuwa, shambulio hilo siku ya Jumanne katika mji huo mdogo lilianza baada ya watu 200 wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Boko Haram wakiwa na silaha nzito kuwasili katika mabasi na magari madogo saa 11 alfajiri.
Msemaji huyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, baadhi ya watu hao wenye silaha walishambulia kambi za jeshi lakini walirudishwa ambapo kumi kati yao waliuawa na wawili kukamatwa.

Polisi pia wauwa

“Lakini watu hao walivamia gereza , na kuwaachilia wafungwa 105, na kuwauwa walinzi wote wa gereza waliokuwa nje isipokuwa wale waliojificha ndani ya stoo ya ya kuhifadhia vyombo vya kupikia,” ameongeza.
Baadhi ya washambuliaji hao walivalia sare maalum za kijeshi na walishambulia kwa takriban saa tano.
Maafisa wa polisi 22, walinzi 14 wa gereza, wanajeshi wawili na raia wane inasemekana wameuawa katika shambulio hilo pamoja na wafuasi 13 wa Boko Haram.
Kamanda wa polisi wa Bama, Abubakar Sagir amekaririwa akisema kuwa, miongoni mwa raia hao walikuwemo watoto watatu na mwanamke mmoja.
Kama linavyofahamika, kundi la Boko Haram, lina mizizi yake katika mkoa huo wa Nigeria. Linapigana kuipindua serikali ili kuunda taida la Kiislamu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, jeshi la Nigeria lilianzisha mashambulizi ya kuwasaka wanamgambo hao katika majimbo ya Baga na Borno, baada ya wapiganaji wa Boko Haram kushambulia msafara wa kijeshi.
Watu wapatao 200 waliuawa katika msako huo na maelfu ya majengo kuharibiwan hali iliyosababisha makundi ya kutetea haki za binadamu kudai kuwa, jeshi lilitumia nguvu kupita kiasi. Jeshi lilitangaza kuwa watu waliokufa walikuwa 37.

BBC - SWAHILI

ICC yaahirisha kesi dhidi ya makamu wa rais wa Kenya

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) siku ya Jumatatu (tarehe 6 Mei) iliahirisha kuanza kwa kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, ikisema kuna masuala kadhaa ya kiutawala ambayo yanahitajika kuwekwa sawa, liliripoti shirika la habari la AFP.
"Jopo limebadilisha tarehe ya kesi ya Mei 28, 2013," lilisema jopo la majaji watatu kwenye uamuzi uliofikiwa makao makuu ya mahakama hio, The Hague. "Tarehe mpya ya kuanza kwa kesi...itatajwa kwa muda muafaka."
Ruto, mwenye umri wa miaka 46, anakabiliwa na mashitaka matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa dhima yake katika ghasia zilizozuka Kenya baada ya uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2007.
Mwezi uliopita, waendesha mashitaka waliomba kuongeza mashahidi watano kwenye orodha yao, jambo lililowafanya mawakili wa Ruto kuomba mkutano wa kuangalia hadhi kujadiliana maendeleo ya kesi hiyo. Mawakili wa Ruto pia waliiomba mahakama kuahirisha kesi hadi angalau mwezi wa Novemba ili kuwapa muda wa kujitayarisha vyema.
Majaji wa ICC waliahirisha kesi ya Ruto mara moja hapo kabla, wakisema kwamba wanachukulia ni muhimu kwa mshitakiwa kuwa na wakati wa kutosha ili kuitayarisha vyema kesi yake.
Ruto atakwenda kesini na mshukiwa mwenzake, mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang.
Mapema mwezi Machi, majaji pia waliiahirisha kesi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta hadi tarehe 9 Julai. Wote wawili, Ruto na Kenyatta, wanakana mashitaka hayo.