Rais wa Ujerumani Joachim Gauck leo (09.05.2013) anaanza ziara ya siku tisa katika bara la Amerika Kusini, ambayo itampeleka kwanza Colombia na baadae Brazil, mshirika muhimu zaidi wa Ujerumani Amerika ya Kusini.
Akiwa nchini Brazil, ambayo ndiyo taifa la sita kwa uchumi mkubwa duniani, Gauck anatarajiwa kujikita katika masuala ya kiuchumi, na nchini Colombia atazungumzia haja ya maridhiano ya kitaifa. Serikali ya Colombia kwa sasa inashiriki mazungumzo na kundi la waasi wa "Revolutionery Armed Forces of Colombia" FARC, mchakato ambao kwa mara ya kwanza umeonyesha matumaini ya kufanikiwa. Mgororo wa nchi hiyo uliodumu kwa nusu karne sasa, umegharimu maisha ya watu karibu laki mbili, na kusababisha wengine milioni 4 kuyakimbia makaazi yao.
Rais wa Colombia, Juan Manuel Santos.
Gauck ambae ni mchungaji wa zamani wa kilutheri na mwanaharakati wa
kupinga ukomunisti kutoka Ujerumani ya Mashariki, ana uzoefu mkubwa
katika mchakato wa ushirikishwaji na anatarajiwa kuzungumzia suala hilo
mara nyingi wakati wa ziara yake. Ujerumani inajiona kama mshirika
katika mdahalo wa Colombia, na imekuwa ikielekeza msaada wake kwa
uendelezaji wa mchakato wa amani. Ingawa hali ya haki za binaadamu
nchini humo haiwezi kuchukuliwa kama isiyo na matatizo, serikali ya rais
wa Colombia Juan Manuel Santos inachukuliwa kuwa katika njia sahihi kwa
mujibu wa ofisi ya rais wa Ujerumani.Maridhiano miongoni mwa jamii ya Wacolombia ni sharti la kupatikana kwa mafanikio ya kiuchumi. Serikali ya Ujerumani imeikubali Colombia kuwa miongoni mwa shabaha zake za masoko, na nchi hiyo ndiyo mshirika mkuu wa Kibishara wa Colombia katika bara la Ulaya, na kimataifa, ujerumani ni nchi ya nne nyuma ya Marekani, China na Mexico.
Uchumi kuzungumzwa Brazil
Rais Gauck ataizuru Brazil siku ya Jumapili, ambapo masuala ya kiuchumi ndiyo yatakuwa kwenye ajenda yake. Ziara yake mjini Sao Paulo itaashiria kuanza kwa mwaka wa Ujerumani katika taifa hilo la Amerika Kusini, ambao mtangulizi wa Gauck Chritian Wulff alikubaliana na Rais wa Brazil Dilma Rousseff kuuanzisha mei 2011.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameizuru Brazil mara moja tu katika uongozi wake, mwaka 2008. Mwaka uliyopita, alifuta ushiriki wake katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu, maarufu kama Rio+20, jambo lililowasikitisha Wabrazil. Jumuiya ya wafanyabiashra wa Ujerumani nchini Brazil wangependa kumuona Merkel tena, kwa sababu nchi hiyo ndiyo mshirika imara zaidi wa kiuchumi wa Ujerumani katika Amerika ya Kusini, na Gauck anatizamiwa kusafisha njia kwa ajili ya ziara hiyo.
Rais wa Brazil, Dilma Rousseff.
Gauck anaongoza ujumbe mkubwa wa kiuchumi, unaojumlisha wataalamu wa
mazingira na teknolojia ya dawa, uhandisi, usafiri wa anga na
usafirishaji, pamoja na wawakilishi wa sekta ya ujenzi na usanifu
majengo. Wafanyabiashara wa Ujerumani wanatumaini kushiriki katika
miradi ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mashindano ya kombe la
dunia mwaka 2014, na michezo ya olimpiki mwaka 2016 na pia katika
upanuzi wa bandari za nchi hiyo.Kuna karibu makampuni 800 ya Ujerumani yanayoendesha shughuli zake katika mji wa Sao Paulo peke yake. Mji huo unaoshikilia uchumi wa Brazil ndiyo unaochukuliwa kuwa na shughuli nyingi za viwanda vya Kijerumani nje ya Ujerumani. Lakini uchumi wa nchi hiyo ulipungua kasi na kufikia kiwango cha ukuaji cha asilimia 0.9 tu mwaka uliyopita, huku mfumuko wa bei ukiwa asilimia 5.8, na unatarajiwa kuendelea kuwa katika kiwango hicho mwaka huu.