Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif anaendelea kuongoza katika uchaguzi wa bunge nchini Pakistan, kwa mujibu wa matokeo ya awali leo
Sharif aliangushwa kutoka
madarakani katika mapinduzi mwaka 1999, akafungwa
na kupelekwa kuishi uhamishoni. Nawaz ameweza
kurejea tena kwa kishindo na kupata
ushindi katika uchaguzi na leo Jumapili (12.05.2013)
anaelekea kupata uongozi kwa kipindi cha tatu
katika uchaguzi mkuu kama waziri mkuu wa
Pakistan.
Kituo cha binafsi cha
televisheni cha Geo kimeripoti kuwa chama cha
Nawaz cha Pakistan Muslim League-Nawaz (PML-N) kinaongoza
katika majimbo 126 ya ubunge kati ya
majimbo 268 yanayowaniwa.
Kituo
cha televisheni cha Dunya kimesema kuwa
chama cha PML-N tayari kimepata viti 80. Kituo
cha taifa cha televisheni nchini Pakistan pia
kimesema chama hicho kinaongoza.
Matokeo ambayo si rasmi yanaonesha
kuwa chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf cha mchezaji
wa zamani nyota wa mchezo wa kriketi
Imran Khan kiko katika nafasi ya pili.
Chama tawala cha zamani cha Pakistan
Peoples Party cha rais Asif Ali Zardari
kinafuatia.
Vyama vya
kidini havikufua dafu
Vyama vya kidini vyenye mtazamo
wa mrengo wa kulia vimeshindwa kupata
mafanikio ya maana.
Maafisa wa uchaguzi wamesema kuwa
watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni
kiasi ya asilimia 60 ya wapiga kura milioni
86 wenye haki ya kupiga kura , ikiwa ni
idadi kubwa kuwahi kujitokeza kupiga kura.
Asilimia 44 tu ya wapiga kura walijitokeza
katika uchaguzi mkuu mwaka 2008.
Uchaguzi wa kihistoria
Uchaguzi huo ni wa kwanza katika
historia ya nchi hiyo , ambapo kunafanyika
mabadiliko kwa njia ya kidemokrasia kutoka
utawala mmoja wa kiraia kwenda kwenda
kwa mwingine.
Mkuu wa tume ya uchaguzi
Fakhruddin Ibrahim amejiita "mtu mwenye furaha",
baada ya kutangaza kuwa uchaguzi huo
umefanyika kwa uwazi.
"Sasa mpira uko upande wenu,
mtaamua kupata serikali yenye utawala mzuri,"
jaji huyo mstaafu ameuambia mkutano na
waandishi wa habari mjini Islamabad.
Ghasia
Ghasia za siku ya uchaguzi
hata hivyo zimesababisha vifo vya watu 28
na wengine 91 wamejeruhiwa katika
mashambulio ya mabomu pamoja na mashambulio
yaliyolenga maeneo maalum.
Kwa
jumla viti 272 vinagombaniwa katika
bunge la taifa , baraza la wawakilishi
ambalo lina jukumu la kuunda serikali. Katika
majimbo manne ya uchaguzi , uchaguzi umefutwa
kutokana na sababu za kiusalama.
Uchaguzi huo pia unajumuisha viti
577 katika mabunge manne ya majimbo.