Mabao mawili ya Frank Lampard yaliifanya Chelsea kuibuka na ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya Aston Villa.
Magoli hayo mawili
aliyoyafunga Lampard ambaye ni nahodha msaidizi wa timu hiyo na timu ya taifa
ya Uingereza, yamefanya avunje rekodi ya Bobby Tambling mchezaji wa zamani wa
Chelsea na kuweka rekodi mpya ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo
ya mashariki mwa London baada ya kufikisha idadi ya kufunga jumla ya mabao 203
tangu aanze kuichezea The Blues.
Chelsea walikuwa
wageni kwenye uwanja wa Villa Park katika mechi ambayo ilikuwa na ushindani
huku kadi mbili nyekundu zikitoka.
Christian Benteke wa
Aston Villa na Ramires wa Chelsea walipewa kadi nyekundu kwa nyakati tofauti.
Kwa matokeo haya
Chelsea sasa wanasalia kwenye nafasi ya tatu na pointi 72 huku Aston Villa
wakiwa bado kwenye nafasi ya 13 na pointi 40.
Michezo mingine ya
ligi kuu ya England inayofikia tamati wiki ijayo itachezwa kwa nyakati tofauti
hapo jumapili.
Stoke City watakuwa
wakipambana na Tottenham Hotspurs wakati Everton watakuwa nyumbani
kuwakaribisha West Ham United.
Kwingineko Fulham
watawakaribisha Liverpool kwenye uwanja wa Craven Cottage huku Norwich
wakitarajia kupapatauana na West Brom.
Sunderland wao
watakuwa wakicheza mchezo ambao kocha wao Paulo Di Canio ameuita mchezo wa
fainali kwao dhidi ya Southampton,mchezo ambao utaamua hatima yao ya kushuka
ama kusalia kwenye ligi kuu msimu ujao.
Mabingwa Manchester
United wao watacheza mchezo wao wa mwisho kwenye uwanja wa Old Trafford dhidi
ya Swansea, mchezo ambao United watautumia kumuaga kocha wao Sir Alex Ferguson
aliyetangaza kustaafu msimu ujao na pia watakuwa wakikabidhiwa rasmi kombe la
ubingwa wa ligi kuu msimuu huu.
Na mchezo wa mwisho
QPR watakuwa wakipambana na Newcastle, mchezo ambao BBC Ulimwengu wa soka itakuwa
ikutangazia moja kwa moja kuanzia majira ya saa kumi na moja na nusu jioni kwa
saa za Afrika mashariki sawa na saa kumi na nusu Afrika ya kati.
BBC - SWAHILI.