Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ametangaza hali ya hatari katika majimbo matatu nchini humo, na kuamrisha wanajeshi zaidi wapelekwe katika majimbo hayo ili kukabiliana na kundi la Kiislamu la Boko Haram.
Kundi lenye msimamo mkali wa dini ya Kiislam la Boko Haram limezidisha mashambulizi dhidi ya vyombo vya usalama na shabaha za serikali katika ngome yake kaskazini-mashariki mwezi huu, hali iliyomlaazimu rais Jonathan kutangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa.
"Baada ya mashauriano mapana, na kwa kutumia mamlaka niliyonayo chini ya vifungu vya ibara ya tatu, kifungu kidogo nambari moja cha katiba ya Nigeria ya mwaka 1999 kama ilivyofanyiwa marekebisho, natangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa," alisema rais Jonathan katika hotub yake iliyotangazwa moja kwa moja na vituo vya redio na televisheni.
Mgogoro wa viongozi wa kaskazini
Rais Jonathan pia alimuagiza mkuu wa majeshi nchini humo kupeleka vikosi zaidi katika majimbo hayo, katika hatua ambayo inaweza kumtumbukiza katika mgogoro na magavana wenye nguvu na viongozi wa kaskazini, ambao tayari ana uhusiano wa mashaka nao. Siku ya Jumatatu, jukwa la magavana wa Nigeria, ambalo linawakilisha magavana wa majimbo 36 ya nchi hiyo walimuonya Jonathan dhidi ya kuweka utawala wa hatari kama jawabu kwa uasi wa Boko Haram.
Maagizo yake yanafuatia ushahidi unaoongezeka kuwa kundi la Boko Haram sasa linadhibiti maeneo kaskazini-mashariki, karibu na ziwa Chad, ambako maafisa wa serikali wameripotiwa kukimbia. Duru za usalama zinasema kundi hilo linadhibiti angalau maeneo 10 ya utawala katika jimbo la Borno, ambalo ndiyo kitovu cha uasi wake.
Boko Haram yadhibiti maeneo kaskazini
Wapiganaji kadhaa wa kundi hilo wakiwa katika mabasi na magari yaliyofungiwa bunduki za rasharasha yaliuzingira mji wa Bama jimboni Borno wiki iliyopita, na kuwaachia wafungwa zaidi ya 100, na kuua watu 55 wengi wao wakiwa maafisa wa polisi na wanajeshi.
Na siku kadhaa kabla, watu kadhaa waliuawa katika kijiji cha uvuvi cha Baga ambacho pia kiko jimboni Borno karibu na ziwa Chad, wakati kijiji hicho kilipovamiwa na vikosi vya Nigeria, Niger na Chad vikiwasaka wapiganaji wa Boko Haram. Wenyeji wa kijiji hicho walisema wanajeshi hao walihusika na mauaji makubwa ya raia.
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau alisema katika mkanda wa video wiki hii kuwa kundi lake limewateka wanawake na watoto wengi katika ulipizaji dhidi ya vikosi vya usalama, ambavyo alisema vinawashikilia wake na watoto wa wanachama wa kundi hilo pasipo na kosa lolote. Shekau pia alikataa pendekezo la rais Jonathan la kutoa msamaha kwa wapiganaji wa kundi, hali ambayo yumkini imechochea amri hii ya hali ya hatari.
Kumekuwepo na ongezeko la vurugu katika majimbo mengine ya Nigeria, ambapo maafisa 46 wa polisi waliuawa na watu wenye silaha katika shambulio la kuvizia katika jimbo la kati la Nassarawa wiki iliyopita, ambapo maafisa walililaum kundi la madhehebu ambalo halihusiki na Boko haramu.
DW - SWAHILI.