Taarifa zinasema, wafungwa 105 walitoroshwa katika shambulio hilo mapema alfajiri lililotokea katika jimbo la Bama, Borno.
Aidha, mashahidi na jeshi linasema kituo cha polisi cha Bama, majengo ya serikali na kambi za kijeshi ziliteketezwa kwa moto.
Habari zinasema, mashambulio ya makundi yenye msimamo mkali ni ya kawaida katika jimbo hilo lakini kiwango cha umwagaji damu kilichotokea katika shambulio la sasa ni cha kutisha.
Mwandishi wa BBC jijini Lagos, Will Ross, anasema shambulio hilo linafuatia mashambulio mengine mabaya siku za nyuma linakinzana na taarifa kwamba, operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo hao zimepunguza tishio la Boko Haram.
Rais Goodluck Jonathan ameunda kamati itakayopitia masharti ya msamaha kwa waasi hao lakini kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, mpaka sasa amekataa wazo hilo.
Msemaji wa jeshi, Musa Sagir, aliyeko mji wa Maiduguri takriban kilomita 70 kutoka Bama, amedai kuwa, shambulio hilo siku ya Jumanne katika mji huo mdogo lilianza baada ya watu 200 wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Boko Haram wakiwa na silaha nzito kuwasili katika mabasi na magari madogo saa 11 alfajiri.
Msemaji huyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, baadhi ya watu hao wenye silaha walishambulia kambi za jeshi lakini walirudishwa ambapo kumi kati yao waliuawa na wawili kukamatwa.
Polisi pia wauwa
“Lakini watu hao walivamia gereza , na kuwaachilia wafungwa 105, na kuwauwa walinzi wote wa gereza waliokuwa nje isipokuwa wale waliojificha ndani ya stoo ya ya kuhifadhia vyombo vya kupikia,” ameongeza.Baadhi ya washambuliaji hao walivalia sare maalum za kijeshi na walishambulia kwa takriban saa tano.
Maafisa wa polisi 22, walinzi 14 wa gereza, wanajeshi wawili na raia wane inasemekana wameuawa katika shambulio hilo pamoja na wafuasi 13 wa Boko Haram.
Kamanda wa polisi wa Bama, Abubakar Sagir amekaririwa akisema kuwa, miongoni mwa raia hao walikuwemo watoto watatu na mwanamke mmoja.
Kama linavyofahamika, kundi la Boko Haram, lina mizizi yake katika mkoa huo wa Nigeria. Linapigana kuipindua serikali ili kuunda taida la Kiislamu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, jeshi la Nigeria lilianzisha mashambulizi ya kuwasaka wanamgambo hao katika majimbo ya Baga na Borno, baada ya wapiganaji wa Boko Haram kushambulia msafara wa kijeshi.
Watu wapatao 200 waliuawa katika msako huo na maelfu ya majengo kuharibiwan hali iliyosababisha makundi ya kutetea haki za binadamu kudai kuwa, jeshi lilitumia nguvu kupita kiasi. Jeshi lilitangaza kuwa watu waliokufa walikuwa 37.
BBC - SWAHILI