Wednesday, May 8

Sir Alex Ferguson kustaafu mwisho wa msimu huu.

Sir Alex Ferguson anastaafu akiwa amedumu kwa karibu miaka 27 na karibu michezo 1500 aliyoifundisha Manchester United. Katika taarifa ya United iliyotoka mapema asubuhi ya leo, imesema Uamuzi huo haukuwa jambo dogo kuafikiwa lakini umekuwa ni uamuzi kwa wakati sahihi.
Ndiye meneja mwenye mafanikio zaidi katika historia ya soka la Uingereza ambapo ameshinda mataji 13 ya ligi kuu, Mataji mawili ya Klabu bingwa barani Ulaya na matano ya kombe la FA.
Ferguson ambaye ni raia wa Scotland, mwenye umri wa miaka 71 amehitimisha tetesi ambazo zilikuwa zikivuma tangu jana kuwa huenda angestaafu mwishoni mwa msimu huu na Mchezaji wa zamani wa Manchester United Pad Crerand anasema haujui maisha yatakuwaje Old Traford bila ya Ferguson maarufu kama Fergie.
Uvumi tayari umekwishatanda juu ya nani atakuwa mrithi wake,ambapo meneja wa Everton Mscotland David Moyes ametajwa sana, huku wengine wakimtaja Jose Mourinho na pia taarifa zingine zikimtaja kocha wa Borusia Dortmund Jurgen Kloop japo taarifa hizo zimekanushwa na Klabu hiyo muda mfupi uliopita.
Ferguson atawaaga rasmi mashabiki wa United jumapili ijayo wakati timu hiyo ikikabidhiwa kombe katika mchezo dhidi ya Swansea lakini ataendelea kuwa sehemu ya Manchester United ambapo sasa atakuwa balozi wa heshima wa United na kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo.