Wednesday, May 8

ICC yaahirisha kesi dhidi ya makamu wa rais wa Kenya

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) siku ya Jumatatu (tarehe 6 Mei) iliahirisha kuanza kwa kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, ikisema kuna masuala kadhaa ya kiutawala ambayo yanahitajika kuwekwa sawa, liliripoti shirika la habari la AFP.
"Jopo limebadilisha tarehe ya kesi ya Mei 28, 2013," lilisema jopo la majaji watatu kwenye uamuzi uliofikiwa makao makuu ya mahakama hio, The Hague. "Tarehe mpya ya kuanza kwa kesi...itatajwa kwa muda muafaka."
Ruto, mwenye umri wa miaka 46, anakabiliwa na mashitaka matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa dhima yake katika ghasia zilizozuka Kenya baada ya uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2007.
Mwezi uliopita, waendesha mashitaka waliomba kuongeza mashahidi watano kwenye orodha yao, jambo lililowafanya mawakili wa Ruto kuomba mkutano wa kuangalia hadhi kujadiliana maendeleo ya kesi hiyo. Mawakili wa Ruto pia waliiomba mahakama kuahirisha kesi hadi angalau mwezi wa Novemba ili kuwapa muda wa kujitayarisha vyema.
Majaji wa ICC waliahirisha kesi ya Ruto mara moja hapo kabla, wakisema kwamba wanachukulia ni muhimu kwa mshitakiwa kuwa na wakati wa kutosha ili kuitayarisha vyema kesi yake.
Ruto atakwenda kesini na mshukiwa mwenzake, mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang.
Mapema mwezi Machi, majaji pia waliiahirisha kesi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta hadi tarehe 9 Julai. Wote wawili, Ruto na Kenyatta, wanakana mashitaka hayo.