Mpiganaji wa jihadi aliyezaliwa Marekani, Omar Hammami, anayefahamika pia kama Abu Mansour al-Amriki, aliripotiwa kuuawa na wanajeshi wa al-Shabaab wanaomtii kamanda wa juu wa kundi hilo, Ahmed Abdi Godane, jioni ya Jumanne (tarehe 7 Mei) karibu na kijiji cha Rama Addey kusini mwa Somalia, iliripoti Radio Bar-Kulan inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa.Kwa mujibu wa taarifa ambazo bado hazijathibitishwa, kiongozi wa ngazi ya juu wa al-Shabaab, Fuad Mohamed Qalaf, anayejulikana kama Fuad Shangole, alitoa tangazo hilo jioni ya Jumanne katika hotuba ya jioni baada ya magharibi katika msikiti mmoja wa Bulo Burde mkoani Hiran. Alisema kwamba al-Amriki alivamiwa na mapigano ya risasi yalizuka na kusababisha wanamgambo kadhaa wa al-Shabaab kuuawa.
Katika hotuba yake, Shangole alisema watu waliomuua al-Amriki wametenda kinyume na misingi ya Uislamu, hoja ambayo hapo nyuma ilisemwa na viongozi kadhaa wa juu wa al-Shabaab -- wakiwemo mmoja wa waasisi Ibrahim al-Afghani, kiongozi wa wapiganaji wa kigeni al-Zubayr al-Muhajir na Sheikh Mukhtar Robow Ali (au Abu Mansur) - katika fatwa ya tarehe 30 Aprili iliyokataza kumuua al-Amriki.
Al-Amriki aliwekwa kwenye orodha ya Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) ya magaidi wanaosakwa sana mwezi Novemba na mwezi Machi Marekani ikatangaza zawadi ya dola milioni 5 kwa kichwa chake.
Al-Amriki aliaminika kujificha nchini Somalia na mara kwa mara aliwasiliana na wafuasi wake na wachambuzi wa kimataifa wa masuala ya ugaidi kupitia Twittter katika miezi ya karibuni. Taarifa yake ya mwisho kwenye Twitter ilikuwa ni tarehe 3 Mei baada ya kutuma picha na taarifa kadhaa akiwashutumu wapiganaji wa al-Shabaab wanaomtii Godane kwa kujaribu kumuua.
Katika kipindi cha wiki moja tangu kushindwa kwa jaribio hilo la mauaji, al-Amriki alionekana kuwa na hali ya hatari, akituma taarifa zisizo na shaka juu ya hatari aliyoamini kuwa inamkabili.
"Labda sitaweza kupata tena nafasi ya kutuma taarifa kwenye Twitter lakini kumbuka tu tuliyosema na tuliyoyaamini. Mungu aliniweka hai ili nifikishe ujumbe kwa umma," aliandika hapo tarehe 29 Aprili.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, al-Amriki alituma vidio, nyaraka na taarifa kwenye mitandao ya Twitter na YouTube zinazoeleza kwa undani namna ambavyo uongozi wa al-Shabaab - hasa Godane, anayefahamika pia kama Abu Zubayr -- umekuwa sababu ya kuporomoka kwa kikundi hicho, na jinsi uongozi wa Godane ulivyo kinyume na misingi ya kweli ya jihadi.
Hata kwenye taarifa zake za mwisho kwenye Twitter, al-Amriki aliendeleza mashambulizi yake dhidi ya Godane. "Abu Zubayr ameingiwa na wazimu. Anaanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe," aliandika al-Amriki tarehe 26 Aprili.
Kifo cha al-Amriki hakikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru, na hii si mara ya kwanza kwa habari kama hiyo kusambazwa. Mwezi Aprili 2012, vyombo vya Somalia viliripoti kwamba al-Shabaab ilimuua al-Amriki, ambapo baadaye iligundulika kuwa ni makosa.
SABAHI ONLINE.