![]() |
Kikosi cha Simba sports club |
MABINGWA watetezi, Simba jana ilishindwa kupiga hatua katika mbio za kupunguza pengo la pointi dhidi ya Yanga baada ya kubanwa na sare ya 1-1 na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, beki Shomari Kapombe wa Simba
alishindwa kufunga penalti ya dakika ya 86 ambayo ingeweza kuipa Simba
pointi zote tatu kama ingejaa nyavuni.
Penalti Kapombe ilikuja baada ya Haruna Moshi
kufanyiwa madhambi na Damas Makwaya na kuishia kugonga mwamba wa
pembeni kabla mpira kuokolewa na mabeki wa Ruvu.
pembeni kabla mpira kuokolewa na mabeki wa Ruvu.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa,
Amri Kihemba aliifungia Simba bao la kuongoza kabla ya Ruvu kusawazisha
kwa bao la Nasho Naftal.
Matokeo hayo ambayo hayakufurahiwa na kocha wa
Simba, Patrick Liewig, yanaiacha Simba nyuma kwa pointi sita dhidi ya
Yanga inayoongoza kwa kuwa na pointi 33.
Kocha Liewig ameitetea sare hiyo kwa kusema wachezaji wake kadhaa walikuwa majeruhi hivyo kushindwa kucheza vizuri.
“Tumecheza tukiwa na majeruhi,” alisema Liewig na
kuongeza: “Hata hivyo tulistahili kushinda kwani tulipata nafasi nyingi
za kufunga lakini tukashindwa kuzitumia.”
Katika mchezo huo, timu hizo ziligawana muda wa kutawala mchezo, ambapo Simba walikuwa safi dakika 20 za kwanza.
JKT Ruvu inayonolewa na Kocha Charles Kilinda,
ilitawala dakika 25 za mwisho wa kipindi cha kwanza na kufanya
mashambulizi ya kutosha langoni mwa Simba.
Ruvu waliokuwa wakiongozwa na mchezaji wa zamani
wa Simba Mussa Mgosi na Zahoro Pazi, walifanya mashambulizi mengi kwa
wapinzani wao.
Mrisho Ngassa aliyepumzishwa kipindi cha pili
nafasi yake kuchukukuliwa na Abdallah Juma, alikuwa mwiba kwenye ngome
ya Ruvu akishirikiana na Mwinyi Kazimoto.
Juma alikaribia kufunga bao dakika ya 51 kama siyo kupiga shuti lililomlenga kipa wa Ruvu, Shabaan Dihile kabla ya kutoka nje.