Katika miaka ya karibuni China imekuwa ikitekeleza mkakati wa “kuimarisha taifa kwa sayansi na elimu”, inatilia maanani sana maendeleo ya sayansi na teknolojia na imeongeza fedha katika utafiti wa sayansi na maendeleo ya teknolojia. Mwaka 2003 fedha zilizotumika katika utafiti wa sayansi na maendeleo ya teknolojia zilizidi yuan bilioni 150, ambazo ni 1.35% ya pato yote la taifa.
Hivi sasa mpango wa kuendeleza sayansi na teknolojia unatekelezwa katika sekta ya utafiti wa kimsingi, sayansi na teknolojia ya juu, kilimo, maendeleo ya mashirika ya teknolojia ya kisasa, teknolojia ya anga ya juu na ulinzi wa taifa. Serikali inachagua mashirika kutekeleza mpango huo kwa kufanya zabuni na kutenga fedha za utafiti kwa mashirika hayo.
Kutokana na juhudi za miaka mingi, China imekuwa na uwezo wa utafiti wa sayansi na uvumbuzi wa teknolojia mpya, mafanikio ya utafiti yamefikia au yamekaribia kufikia kiwango cha kisasa cha kimataifa. Mwaka 2003 tasnifu zilizotolewa na wanasayansi wa China zilichukua nafasi ya tano duniani, na hakimiliki za uvumbuzi pia ziliongezeka kwa kiasi kikubwa.