Maafisa nchini Misri wamesema leo kuwa watu saba wameuwawa na wengine 261 wamejeruhiwa katika mapambano kati ya polisi na waandamanaji mjini Cairo jana. Waandamanaji hao wamepambana na polisi jana na leo asubuhi mjini Cairo , baada ya waungaji mkono wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi walipojaribu kuzuwia njia muhimu ya darajani katika mto Nile. Waandamanaji , wengi wao vijana , waliwarushia mawe polisi na kuimba nyimbo za kumsifu Morsi, wakati polisi wakifyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi za mipira. Morsi aliondolewa madarakani na jeshi Julai 3, kufuatia maandamano ya nchi nzima ambapo waandamanaji walikuwa wanadai ajiuzulu. Farid Ismail msemaji wa chama cha Udugu wa Kiislamu, amesema kuwa Marekani inaunga mkono moja kwa moja kuondolewa kwa rais Morsi. Wakati huo huo naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani William Burns ametaka kufanyike majadiliano zaidi nchini humo.
O-Ton William Burns
Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani William Burns amekuwa afisa wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara nchini Misri tangu kuondolewa madarakani kwa rais Morsi . Burns amekosoa hatua ya waendesha mashtaka wa serikali kuwakamata viongozi waandamizi wa kundi la Udugu wa Kiislamu.