Wednesday, July 3

Obama ahitimisha ziara ya Afrika


Rais wa Marekani Barack Obama amehitimisha ziara yake barani Afrika nchini Tanzania huku akikutana na mtangulizi wake George W. Bush katika kumbukumbu ya wahanga wa mashambulizi ya ugaidi mwaka 1998 mjini Dar es Salaam.
Rais Obama na familia yake walikuwa jijini Dar es Salaam katika siku ya mwisho ya ziara iliyodumu wiki nzima, wakati Bush na mkewe Laura wapo jijini humo kama wenyeji wa mkutano kuhusu nafasi ya wake wa marais katika kuleta mabadiliko nchini mwao. Bush aliungana na rais Obama katika hafla ya kuweka maua kuwakumbuka wahanga wa Kitanzania wa mashambulizi yaliyotokea wakati mmoja dhidi ya balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwezi Agosti 1998, ambayo yanadaiwa kupangwa na Osama bin Laden.Marais hao wawili waliinamisha vichwa vyao wakati mwanajeshi wa majini akiweka maua ya rangi nyekundu, nyeupe na bluu katika kumbukumbu hiyo. Baada ya dakika chache, wawili hao walishikana mikono na manusura wa mashambulizi hayo pamoja na jamaa za waliouawa kabla ya kurejea tena ubalozini baada ya dakika chache tu.
Wake zao nao washiriki mjadala
Wakati huo, wake zao walikuwa wakishiriki katika mjadala wa umma uliokuwa ukiendeshwa na mwandishi wa habari wa Kimarekani Cokie Roberts. Mke wa Obama alisema alitaka kuonekana na Laura Bush kwa sababu "nampenda mwanamke huyo." "Ni kama klabu fulani ya wanafunzi wa chuo kikuu nadhani," alijibu Laura Bush kimaskhara. Lengo lao lilikuwa kuwahimiza wake wa marais wa Afrika, ambao wengi wao walikuwepo katika hadhira, kupandisha sauti zao kwa ajili ya mambo walio na mapenzi nayo.
Wakati watu wakichambua viatu vyetu na kushughulikia nywele zetu--" alianza mke wa Obama. " Hata tukiwa na mabango," aliingilia kati Laura Bush na kusababisha kicheko. Michelle alionyesha kustajabishwa kuwa mfumo wa nyewele zake unavutia waandishi wengi wa habari. "Nani angefikiria hivyo?" Laura alisema anampa pole Michelle kwa sababu hata nyewele za binti yake Barbara zilisababisha msukosuko wakati fulani.
Lakini Michelle Obama alisema mwishowe watu wanaancha kuangalia mabango yao na kuanza kuangalia kile walichosimama mbele yake. Akiwa barani Afrika, Obama amemsifu Bush mara kwa mara kwa kusaidia kuokoa mamilioni ya maisha kwa kufadhili matibabu ya ugonjwa wa ukimwi. "Napenda kumshukuru tena nikiwa katika ardhi ya Afrika kwa niaba ya watu wa Marekani, kwa kuonyesha jinsi ukarimu wa wamarekani na muono wa mbali vinavyoweza kubadilisha maisha ya watu," alisema Obama siku ya Jumatatu.Washirika badala ya wafadhili
Lakini rais huyo alisema pia anataka kubadilisha mkakati wa Marekani kwa Afrika. "Tunatafakkari kuwa na ruwaza mpya ambayo msingi wake si tu msaada, bali pia ushirikiano wa kibiashara," alisema. "Mwisho wa siku, lengo hapa ni kwa Afrika kuijenga Afrika kwa ajili ya Waafrika," Obama alisema na kuongeza kuwa kazi yao kama Wamarekani ni kuwa washirika katika mchakato huo.
Katika moyo huo, Obama alitangaza mkataba mpya wa kibiashara na mataifa ya kanda ya mashariki mwa Afrika, na programu ya kuongeza upatikanaji wa umeme kwa Waafrika wasiokuwa na nishati hiyo. Ugunduzi mmoja unaoweza kusaidia katika suala la umeme ni "Soccket ball," ambao ni mpira uliyogunduliwa na wasomi wawili wa chuo kikuu cha Harvard. Mpira huo una mtambo ndani yake unaofanana na penduli, ambao unafua nishati mwendo wakati unachezwa na kuihifadhi. Watengenezaji wake wanasema ukichezwa kwa dakika 30 unaweza kuwasha taa ya LED kwa masaa matatu. Mpango ni kuisambaza mipira hiyo kwa watoto barani Afrika.Programu ya Power Africa
Wakati wa ziara yake katika mtambo wa umeme wa Ubungo na rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, Obama aliupiga mpira huo, na kusema kuwa mipira hiyo itaanza kusambazwa kote barani Afrika. Mtambo huo wa Ubungo ulidhaminiwa kwa mkopo usio na riba kutoka Marekani na kujengwa na kampuni ya Marekani ya American Corpration General Electric and Symbion.
Katika hotuba yake baada ya ziara hiyo, Obama aliipigia debe programu ya umeme ya 'Power Africa' akiita kuwa ni ushindi kwa makampuni ya Afrika na ya Marekani. Pia alizungumzia ziara yake ya wiki nzima, na kukumbuka baadhi ya watu aliokutana nao njiani, akiwemo mkulima mmoja wa kike nchini Senegal na vijana mjini Soweto. "Nimetiwa moyo kwa sababu nimeshawishika kuwa ikiwa njia sahihi zitafuatwa, Afrika na watu wake wanaweza kuanzisha enzi mpya ya mafanikio," alisema Obama.