Rais wa Marekani Barack Obama alipata mapokezi ya shangwe na furaha Jumatatu (tarehe 1 Julai) katika ziara yake ya kwanza nchini Tanzania, nchi ya tatu na ya mwisho katika ziara ndefu Afrika.Obama alilakiwa jijini Dar es Salaam na umati mkubwa kwa ziara yake na maelfu ya watu -- baadhi wakiwa wamevaa fulana na nguo za asili zenye picha yake -- walijipanga barabarani wakati msafara wake ukipita. Kwa heshima ya ziara ya kihistoria, barabara ya kando ya bahari inayoelekea kwenye makazi ya rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, imebadilishwa jina na kuitwa jina la kudumu la Barabara ya Barack Obama.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mazungumzo rasmi, Kikwete alimshukuru Obama kwa kukubali mwaliko wa kutembelea Tanzania na uwajibikaji wake katika kuendelea kusaidia maslahi ya nchi hizi mbili.
"Umejionea mbubujiko wa furaha," Kikwete alisema. "Hakujawahi kuwa na ziara ya mkuu wa nchi nchini Tanzania ambayo ilivutia umati mkubwa wa watu kama [hii] -- Ni ya kipekee."
Ziara hii imekuja katika kipindi cha kumbukumbu ya miaka 50 ya uhusiano baina ya Tanzania na Marekani, wakati Rais wa Marekani John F. Kennedy alipomkaribisha Ikulu ya Marekani rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere.
Obama alitumia nafasi hii kutangaza jitihada za sera ya uchumi ya Marekani kwa Afrika na kusisitiza juu ya ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania. Pia alisifu jitihada za Tanzania katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kuboresha utoaji wa huduma.
"Kwa hatua sahihi, Tanzania ina umuhimu wa kufungua ukuaji mpya wa kiuchumi siyo tu katika nchi hii lakini katika Afrika Mashariki yote," Obama alisema.
"Kwa mfano, Watanzania wanaendelea kufanya kazi ya kuimarisha demokrasia yao. Bunge, vikundi vya upinzani, vikundi vya vyama vya kiraia na waandishi wa habari wote wanatimiza wajibu wao kupata utawala bora na uwazi ambavyo vinategemewa na demokrasia na mafanikio."
Obama alimsifia Kikwete, Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na watu wa Tanzania kwa "kuingia katika mchakato muhimu wa katibaambao utaamua mustakabali wa taifa hili na demokrasia yake."
Katika mkutano kabla ya marais wawili kuhutubia wananchi, Obama na Kikwete walijadiliana masuala kadhaa muhimu na mipango ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo Tanzania, ambayo inaajiri idadi kubwa ya Watanzania.
Programu ya Serikali ya Marekani ya Feed the Future imesaidia wakulima zaidi ya 14,000 wa Tanzania kuweza kusimamia vizuri mazao yao na kuongeza mavuno kwa takribani asilimia 50, Obama alisema. "Hii inamaanisha kipato kikubwa na ngazi ya familia na jamii kupata mafanikio makubwa," alisema.
Kikwete na Obama pia walijadili kutoa fursa ili kuwasaidia vijana wa Tanzania kuanzisha makampuni mapya na kuleta ajira mpya. Walijadili uwekezaji Tanzania katika barabara mpya na zilizoboreshwa, kuboresha upatikanaji wa maji na marekebisho ya sekta ya nishati, ambavyo Obama alisema "vinaweza kusaidia kuwaondoa watu katika umasikini na kufungua ukuaji wa uchumi."
Viongozi hao wawili walikubaliana kuendelea kushirikiana kupunguza wagonjwa wa malaria na vifo vya watoto, pamoja na VVU/UKIMWI.
Obama alimshukuru Kikwete kwa mchango wa Tanzania katika usalama wa kanda, pamoja nakupeleka vikosi vya kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Darfur. Marais hao wawili walikubaliana "vikundi vyenye silaha vinahitaji kuweka chini silaha zao na wanaokiuka haki za binadamu wanatakiwa kuwajibishwa".
Pia walizungumzia uhifadhi wa wanyamapori na sekta ya utalii, ambavyo vinatishiwa na ujangili na biashara haramu. Obama aliahidi "mamilioni ya dola kuzisaidia nchi katika kanda kujenga uwezo wao ili kukabiliana na changamoto hiyo, kwa sababu dunia nzima ina wajibu wa kuhakikisha kwamba tunalinda uzuri wa Afrika kwa ajili ya kizazi kijacho".
Nishati Afrika, Biashara Afrika
Tangazo kuu la safari ya Obama nchini Senegal, Afrika Kusini na Tanzania lilikuwa ni mpango wake wa "Umeme Afrika" , ambao unalenga upatikanaji mara mbili wa umeme katika Afrika.
Serikali ya Marekani imeahidi zaidi ya dola bilioni 7 kwa ajili ya mradi huo kwa miaka mitano ijayo, ilahli makampuni ya sekta binafsi ya Marekani, Ulaya, Afrika na Asia yaliahidi zaidi ya dola bilioni 9 ili kusaidia uzalishaji wa megawati zaidi ya 8,000 za uzalishaji mpya wa umeme katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mpango wa "Umeme Afrika" utajenga uzalishaji mkubwa wa nishati Afrika, pamoja na ugunduzi mpya wa akiba kubwa ya mafuta na gesi, na matarajio ya nishati ya ardhini, maji, upepo na umeme wa jua," Ikulu ya Marekani ilisema katika taarifa yake ya tarehe 30 Juni.
Wakati wa mkutano na wafanyabiashara katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam Jumatatu usiku, Obama alitangaza shughuli nyingine iliyoitwa "Biashara Afrika" ili kuongeza biashara na Afrika na ndani ya Afrika, ikianza na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
"Afrika ni mahali ambako uchumi unaokuwa kwa kasi duniani," alisema. "Sekta kama rejareja, mawasiliano ya simu na uzalishaji zinakua kwa kasi. Na hapa Afrika Mashariki, kwa muongo, uchumi wake umeongezeka mara nne. Dunia inawekeza Afrika kuliko wakati wowote hapo kabla."
Ukuaji huo unabadilisha maisha, alisema, kuongeza kipato na kupunguza kiasi cha umaskini, lakini inatakiwa kuwa rahisi kufanya biashara Afrika.
"Bado inachukua muda mrefu -- nyaraka nyingi, urasimu mwingi kupita kiasi -- kuanzisha biashara tu, kujenga mtambo mpya, kuanza kuuza nje ya nchi," alisema. "Hakuna anayetakiwa kulipa hongo ili aanzishe biashara au kusafirisha bidhaa zao."
Biashara itaelekea ambako sheria zinaeleweka, uwekezaji unalindwa na umeme ni wa uhakika, alisema Obama.
Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo aliupongeza mpango wa Umeme Afrika na athari zake kwa Tanzania. "Nchini Tanzania mpango huo utasambaza umeme kwa watu milioni 20," Muhongo aliiambia Sabahi.
Obama alihitimisha maoni yake siku ya Jumatatu kwa kusema watu ni rasilimali kubwa ya Afrika.
"Kama watu katika bara hili watapewa nafasi, kama watawezeshwa kwa ujuzi na rasilimali na mtaji -- na serikali zikaharakisha na kuendeleza fursa kinyume na kuwa kikwazo -- wanaweza kufanikiwa kwa maendeleo ya ajabu kabisa," alisema.
Kuwakumbuka waliofariki
Kabla ya kurejea Washington siku ya Jumanne, Obama aliungana na Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush kuwakumbuka waliouawa katika mlipuko wa ubalozi wa Marekani nchini Tanzania mwaka 1998.
Katika mkutano wa nadra wa viongozi wa Marekani ugenini, Obama na Bush walisimama wakitazamana na kuinamisha vichwa vyao katika hali ya ukimya kuwakumbuka waathirika wa mlipuko huo, jiwe la msingi katika uwanja mpya wa ubalozi wa huko Dar es Salaam, AFP iliripoti.
Eneo halisi lililolipuliwa na al-Qaeda na kuua watu 11, liko umbali wa maili moja na nusu kutoka maeneo ya ubalozi mpya wa Marekani.
Watanzania kumi na tano waliokuwa wakifanya kazi katika ubalozi na kupona dhidi ya shambulio hilo bado ni wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani hadi leo, Ikulu ya Marekani ilisema.
Ulipuaji wa bomu ulipangwa kufanyika kwa wakati huohuo katika ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Nairobi nchini Kenya ambako ulisababisha vifo vya watu 213 na wengine maelfu kujeruhiwa.
Chanzo:sabahionline