Sunday, February 10

Imani za kishirikina zatawala AFCON South Africa


WAAFRIKA na imani za kishirikina ni kama mapacha. Inaonekana kwa baadhi ya Waafrika kuacha imani za kishirikina ni jambo ambalo haliwezekani kwani hali hiyo imejitokeza katika Fainali za Afrika zinazoendelea nchini Afrika Kusini.
Mashabiki wa Ghana, DR Congo na Niger wanapanga kupeleka malalamiko yao kwa waandaaji wa Fainali za Afrika 2013 ili kuwazuia wanawake wasiwasogelee wachezaji wao kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Bay zinazoutumia uwanja huo.
Tayari mashabiki hao wameishawafuata walinzi wa uwanja huo na
kuwaambia wasikubali wanawake kukaribia vyumba vya kubadirishia nguo wachezaji.
“Tumeambiwa tuwazuie wanawake kukaribia vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji kwa sababu nchi za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati zinaamini wanawake
katika soka ni nuksi na wanahusishwa na ushirikina,”alisema mlinzi mmoja wa uwanja huo.
Hata hivyo kamishna anayehusika na usawa wa jinsia katika Kamati inayoshughulikia kuandaa fainali hizo, Javu Baloyo alisema imani hizo za kishirikina hazina nafasi na wanawake wasizuiwe.
“Wanawake wanaenda katika mechi za soka kwa ajili ya kushangilia timu zao na siyo kuwasumbua wachezaji, kushinda au kupoteza mechi hakutakiwi kuhusisha wanawake,”alisema Baloyo.
Shabiki mmoja wa kike wa soka wa Afrika Kusini alisema,”kitendo kilichofanywa cha kutuzuia kuwa huru uwanjani siyo sahihi, pia wanawake tumeshushwa hadhi zetu, tumetukanwa na tunaona tumerudishwa katika enzi zile za ubaguzi wa rangi.”
Naye ‘Sangoma’ mganga mmoja wa kienyeji nchini Afrika Kusini anayeitwa, Bhayilatsholoza Mngambe alisema,”wanawake wanatakiwa kuzuiwa kabisa kuingia viwanjani, kwa mujibu wa tamaduni za kiafrika, wanawake hawatakiwi kuwa karibu na wanajeshi wakati wa vita, Fainali za Afrika ni sawa na vita.”