Thursday, February 14

Eto'o: Niliogopa kuuawa ndio maana sikuja Tanzania

Samuel Eto'o Fils - Cameroon
MASHABIKI wa soka nchini walitoka mikoani kuja Dar es Salaam ili kumwona nyota wa Cameroon, Samuel Eto'o timu yake ilipocheza mechi ya kirafiki na Taifa Stars Uwanja wa Taifa, Jumatano iliyopita.

Lakini hakuja na timu yake ikalala bao 1-0. Benchi la ufundi la Cameroon likadanganya Watanzania kwamba straika huyo alikuwa majeruhi. Kumbe ni uongo.

Sasa yeye mwenyewe ameibuka na kutamka kuwa aligoma kuja nchini kutokana na kuhofia kuuawa.

Nahodha huyo ameibua mjadala mzito baada ya kuwatuhumu maofisa wa Shirikisho la Soka la Cameroon (FECAFOOT) kwa kutaka kumuua.

Sambamba na kauli hiyo, Eto'o, amesema kwamba yuko tayari kwa mjadala wa suala hilo ambao utarushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya taifa.
Wanataka kuniua, katika timu ya taifa naishi na

mashushushu, si kwamba siko makini katika hilo kwani hata jezi ya timu ya taifa navaa yangu binafsi niliyotengenezewa na Puma, alisema mchezaji huyo kupitia Jarida la Je Wanda.

Etoo ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi pia alisema kwamba hata anapokuwa mazoezini wakati wote yuko makini na maisha yake.

Etoo ni miongoni mwa wachezaji 11 wa Cameroon ambao hawakuitikia wito wa kuichezea timu hiyo mechi ya kirafiki dhidi ya Tanzania iliyopigwa Jumatano iliyopita na Cameroon kulala bao 1-0 lililofungwa na Mbwana Samatta.
Hawa wazee wametafuna fedha zetu kiasi cha kutosha, badala ya kusimamia soka kwa ajili ya umma wako katika mipango ya uongo, kusafiri daraja la kwanza kwenye ndege na kunufaisha akaunti zao za siri katika mabenki ya Ulaya, alisema.

Cameroon itaumana na Togo mwezi ujao katika mechi ya awali ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 na Etoo anadhani timu hiyo haina uwezo wa kuifunga Togo.

FECAFOOT haijasema lolote kuhusu hoja hizo za Etoo ingawa mmoja wa maofisa wa shirikisho hilo anadaiwa kumwambia Etoo kuwa amekosa uzalendo na hoja zake ni kichekesho.

Kocha wa Cameroon, Jean Paul Akono, alisema jijini Dar es Salaam kwamba anataka kupunguza wachezaji wenye umri na majina makubwa kwenye kikosi hicho na kutengenezakizazi kipya kitakachorejesha heshima ya Taifa hilo kisoka.