Thursday, February 14

Stars yaiponza Cameroon viwango vya ubora wa soka duniani.

Taifa Stars - Tanzania
 TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeiporomosha Cameroon kwa nafasi 12 za ubora wa viwango vya soka vinavyotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).
Taifa Stars iliichapa, Cameroon ‘Indomitable Lion’ bao 1-0, katika mchezo wa kirafiki uliofanyika wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Mchezo ulikuwa ndani ya kalenda ya Fifa.Cameroon iliyokuwa inashika nafasi ya 67, imeporomoka hadi nafasi ya 79 baada ya mchezo huo. Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania, mchezo huo haukuisaidia sana timu hiyo, kwani na yenyewe imeporomoka kwa nafasi tatu.
Kabla ya kutolewa viwango hivyo, Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya 124 na sasa inashika nafasi ya 127 kwa viwango vipya vilivyotolewa jana.

Kwa mujibu wa viwango hivyo vipya, Uganda inaongoza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kushika nafasi ya 84 licha ya kushuka nafasi tatu.
Uganda inafuatiwa na Burundi inayoshika nafasi ya
115 tena ikiwa imeporomoka kwa nafasi 11, huku Kenya ikifuatia ikiwa katika nafasi ya 126 licha ya kupanda nafasi moja.

Rwanda ndiyo ya mwisho katika Ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa nafasi ya 130 baada ya kupanda kwa nafasi saba. Ethiopia iliyoshiriki Fainali za Afrika mwaka huu, imebaki kwenye nafasi yake ya 110 duniani.
Indomitable lion  - Cameroon.

Nigeria iliyotwaa ubingwa wa Afcon mwaka huu, imepanda kwa nafasi 22 hadi 30 lakini imeshindwa kuipiku Ivory Coast inayoshika nafasi ya 12 wakati Ghana iko nafasi ya 19 huku Mali ikishika nafasi ya 25.

Algeria inashika nafasi ya 34 wakati waliokuwa mabingwa wa Afrika mwaka jana, Zambia inashika nafasi ya 47.

Tunisia ni ya 42, Jamhuri ya Afrika ya Kati (51), Burkina Faso (55) na Afrika Kusini waliokuwa wenyeji wa Afcon wanakamata nafasi ya 65.

Hispania ambao ni mabingwa wa Kombe la Dunia na Ulaya wanaendelea kuongoza kwa kushika nafasi ya kwanza katika viwango vya Fifa, wakifuatiwa na nchi za Ujerumani, Argentina, England, Italia, Colombia, Ureno, Uholanzi, Croatia na Urusi.