Tuesday, February 19

Watoto masikini waachwa nyuma kwa sababu ya elimu ya gharama za juu huko Mogadishu.

Yusuf Bilow Isaq, mwenye umri wa miaka 41, mfanyabiashara ya miswaki katika makutano ya K5 huko Mogadishu, alisema hawezi kumudu kutumia fedha katika elimu wakati familia yake inahangaika.

"Mtoto wangu mkubwa ana miaka 15 na hajawahi kwenda shule na ndugu zake wadogo wako katika hali mbaya zaidi kwa sababu hakuna shule za bure," aliiambia Sabahi. "Sina uwezo wa kulipia ada za shule kwa sababu kiasi ninachopata kwa siku ni shilingi 100, ambacho hakiwezi kulipia zaidi ya mahitaji ya kawaida ya familia."
Ingawa shule binafsi zinasaidia kuziba pengo la elimu baada ya kuanguka kwa serikali kuu mwaka 1991, familia nyingi kama ile ya Isaq hazina uwezo wa kifedha. Matokeo yake, watoto wengi katika jiji la Somalia inabidi waachane na
kupata elimu.
"Wakati wowote unapokuwa Mogadishu, unaona mamia ya watoto mitaani," Isaq alisema. "Hawako shuleni kwa sababu familia zao hazina uwezo wa kulipia ada za shule ambazo zinagharimu kiasi kikubwa cha dola 10 kwa mwezi. Kama familia ina watoto watano au sita na inamlipia mtoto mmoja kwenda shule, watoto waliobaki inabidi wakae nyumbani."
Mohamed Yaqub ni baba wa watoto saba mwenye umri wa miaka 45 huko Mogadishu. Aliiambia Sabahi anaihudumia familia yake kama mhudumu, na anamiliki mkokoteni aliyopewa na shirika lisilo la kibiashara.
Yaqub alisema angependa kuwasomesha watoto wake, lakini kati yao hakuna aliyekwenda shule kwa sababu hana uwezo wa kulipia ada.
"Wamiliki wa shule wanajaribu kupata fedha kutoka katika shule zao na hatuna uwezo wa kulipia ada," aliiambia Sabahi. "Watoto wetu hawana elimu kwa sababu chochote tunachopata kwa siku hakiwezi kulipia vyote viwili, elimu na mahitaji mengine ya familia."

Serikali yaahidi kurejesha sekta ya elimu

Abukar Ismail, mwenye umri wa miaka 50, amefundisha kwa miaka 15 na sasa anafanya kazi katika Shule ya Mamur katika wilaya ya Waberi. Alisema serikali inapaswa kujaribu kuboresha hali ya elimu na kurejesha huduma za elimu kupatikana sawa kwa Wasomali wote.
"Familia zinazoishi katika hali ya umaskini zimekuwa sehemu iliyosahaulika ya jamii yetu kwa sababu hawana watetezi wa kufanya kazi badala yao kurekebisha ukosefu wa elimu kwa watoto wao," aliiambia Sabahi.
Ismail alisema kutokuwa na uwezo kwa familia za Somalia na kushindwa kupeleka watoto wao shule kunatokana na ukosefu wa fedha ambalo ni tatizo kubwa la kijamii nchini Somalia.
Mashirika yasiyo ya faida yanaendesha shule chache ambazo zinatoa elimu ya bure kwa wanafunzi, lakini huduma yao inakosa kile kinachohitajika nchini, alisema Abdinasir Yusuf, mwalimu mwenye umri wa miaka 46 katika Shule ya Mohamud Harbi huko Hamar Jajab.
Yusuf alisema tatizo la kupatikana kwa elimu kwa watu maskini linaweza kushughulikiwa kwa kuanzishwa kwa serikali yenye uwezo wa kurejesha huduma zinazotakiwa za elimu.
Mohamed Adan, kiongozi wa Wizara ya Elimu, alisema serikali inatambua tatizo la upatikanaji wa elimu linalowakabili watoto wanaotoka katika familia zinazoishi katika umaskini, na programu zinapangwa kushughulikia suala hilo.
Adan alisema wizara hivi karibuni ilifungua tena Shule ya July 1st huko Howlwadaag. Shule hiyo inafundisha wanafunzi karibia 300, wengi miongoni mwao ni yatima au watoto ambao wazazi wao hawawezi kuhimili ada ya shule. Shule hiyo kwa sasa inatoa elimu ya msingi, ikiwa na mipango ya kuendelea hadi shule ya elimu ya kati hadi elimu ya juu.
"Shule inasimamiwa na serikali ya Uturuki," Adan aliiambia Sabahi. "Kila mmoja anaweza kuwaleta watoto kuhudhuria shule bila masharti kuwekwa kuhusiana na kupata kwao kwa elimu."