Tuesday, February 19

Polisi wa Zanzibari wakamata 3 kwa mauaji ya padre.

Saidi Mwema - IGP.
Polisi wa Zanzibari waliwakamata washukiwa watatu Jumapili kuhusiana na mauaji ya padre wa Kikatoliki Padre Evaristi Mushi, kwa mujibu wa maofisa wa polisi.
Upigwaji risasi ulifanyika saa 1:30 asubuhi mbele ya kanisa la Minara Mwili katika eneo la Mtoni la Zanzibar, mahali ambapo Mushi alikuwa anaenda kufanya ibada ya Jumapili, msemaji wa polisi wa Zanzibari, Mohamed Muhina aliiambia Sabahi.
"Wanaume wawili wenye silaha wakiwa kwenye Vespa [pikipiki] walimtangulia na kumpiga risasi kwenye kichwa," Muhina alisema.
Baadaye siku hiyo hiyo, Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema alisema washukiwa watatu walikamatwa karibu na kanisa.
"Lilikuwa tukio baya na la
kuhuzunisha," Mwema aliwaambia waandishi wa habari. "Kufuatia tukio hili na lililotangulia yanayolenga viongozi wa dini na kuchoma makanisa, kikosi cha polisi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, limeanzisha uchunguzi wa kina katika kutafuta wahalifu hawa."
Naibu kamishna wa polisi Samson Kasala na Peter Kivuyo wataongoza timu hii ya wachunguzi huko Zanzibari.
Mwema alisema polisi haitaweza kuvumilia watu ambao wanatumia dini au tofauti za kidini kuchomeka kabari kati ya jamii na kusababisha maangamizi.
Alisema shambulio hilo linaweza kuwa limeamriwa na al-Qaeda. "Hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa ni al-Qaeda," alisema. "Tupeeni muda tutawaambia [umma] nini hasa tulichogundua baada ya uchunguzi."
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ametoa ruhusa kwa mashirika ya kimataifa ya uchunguzi kusaidia uchunguzi huo, alisema Waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi.