![]() |
Kikosi cha timu ya soka ya Hispania. |
BAADA ya kutua kwa kishindo kwenye fainali mbili za Kombe la Dunia, sasa Hispania inaonekana kubanwa katika safari ya kuelekea Brazil 2014.
Wakati vigogo wenzao walionekana kuwa katika wakati mzuri wa kufuzu katika fainali hizo, Hispania inakwenda uwanjani kupambana na vinara wa Kundi I, Ufaransa mjini Paris huku wakifahamu wakifungwa watakuwa nyuma kwa pointi tano.
Hispania si timu pekee yenye mawazo, licha ya England kushinda mabao 8-0 dhidi ya
San Marino Ijumaa iliyopita itakwenda Montenegro ikiwa nyuma ya wenyeji kwa pointi mbili kwenye Kundi H.
Nayo Ureno ina kazi kubwa ya kufanya ili kufika 'nchi ya ahadi'. Timu hiyo inasafiri kwenda Azerbaijan ikiwa nafasi ya tatu kwenye Kundi F, na haitakuwa na nahodha Cristiano Ronaldo, hiyo inamfanya Paulo Bento kuwa na presha kubwa.
"Tupo kwenye hali mbaya lakini kila kitu kinawezekana. Kuwashinda Azerbaijan ni jambo zuri na tutaendelea kupigana mpaka hatua ya mwisho," alisema beki Joao Pereira.
Hispania ilijikuta ikitoka sare ya bao 1-1 na Finland, Ijumaa iliyopita na Oktoba mwaka jana walitoka sare ya bao 1-1 na Ufaransa. Hiyo imetoa nafasi nzuri kwa Ufaransa ambayo iliichapa Georgia mabao 3-1 Ijumaa iliyopita.
Kitu chochote zaidi ya ushindi kitafanya Hispania ianze kukata tamaa ya kutua Brazil. "Tunafahamu tunakwenda Paris kwa ajili ya kusaka ushindi, hakuna kilichobadilika," alisema mshambuliaji David Villa.
"Matokeo dhidi ya Finland yanatupa sababu ya kusaka ushindi kwa nguvu zote."
Beki wa Arsenal, Nacho Monreal amesema ingawa mechi dhidi ya Ufaransa si fainali, timu yoyote itakayoshinda itakuwa imepiga hatua kuelekea Brazil.
Hispania imeshinda mechi tatu kati ya nne dhidi ya Ufaransa ikiwa ni pamoja na ile ya fainali ya Euro 2012 huko Ukraine, Mara ya mwisho kufungwa ilikuwa ni kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006.
Mechi ya Montenegro na England haishitui kama ile ya Ufaransa na Hispania lakini kikosi cha kocha Roy kitatakiwa kufanya kazi ya ziada kwa kuwa mara ya mwisho walishindwa kuwafunga kwenye mechi za kufuzu Euro 2012, nyumbani na ugenini. Kama wakitoka sare, timu itakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha inaishinda Moldova, Septemba mwaka huu.