![]() |
Fernando Torres - Chelsea fc. |
MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Fernando Torres anataka kurudi Hispania na kuanza maisha mapya kwenye klabu yake ya zamani ya Atletico Madrid.
Habari kutoka kwa rafiki zake wa karibu zinasema kuwa mchezaji huyo anaamini amekosa bahati kwenye kikosi cha Chelsea na suala la kuhamia Atletico ni muhimu kwake.
Wakati mchezaji huyo akifikiria suala hilo, Kocha wa Atletico, Diego Simeone, naye amesema yupo kwenye mipango kabambe ya kumsajili mchezaji huyo katika dirisha la usajili linalokuja.
Kocha huyo ameliambia Jarida la Onda Cero kuwa anafahamu mchezaji huyo anataka kurudi Hispania na
hiyo itamrahisishia kazi ya kumnyakua.
Torres raia wa
Hispania amekuwa na wakati mgumu tangu alipotua Chelsea akitokea Liverpool kwa ada ya pauni 50 milioni mwaka 2011. Imefahamika kuwa mchezaji huyo si tu kwamba hatamani maisha ya kambi ya Chelsea bali hataki hata kuishi England.
Mchezaji huyo mwenye miaka 29 alijiunga na Liverpool mwaka 2007 baada ya kupachika mabao 82 akiwa na kikosi cha Hispania, aliendelea kuwasha moto kwenye kikosi cha Liverpool kwa kufunga mabao 65 katika mechi zaidi ya 100, lakini tangu alipojiunga Chelsea ameshindwa kutamba, amefunga mabao 14 katika mechi 74.
"Fernando Torres kwa sasa anachezea timu nyingine, tunatakiwa kusubiri mpaka mwishoni mwa msimu kuona kama tunaweza kumsajili, lakini tuna matumaini ya kufanya hivyo," alisema kocha huyo.