Wiki mbili zilizopita kumeshuhudiwa maamuzi ya kustaafu kutoka kwa wachezaji kadhaa wa kabumbu nchini Uingereza, na jina la hivi punde kuongeza kwenye orodha hiyo ni David Beckham. Nahodha huyo wa zamani wa Soka ya Uingereza ameamua kustaafu kutoka soka mwisho wa msimu huu.
Beckham mwenye umri wa miaka 38 alijiunga na timu ya Paris
St-Germain ya Ufaransa mapema mwezi wa Januari kwa kandarasi fupi ya miezi
mitano. Wakati wa kutia saini kandarasi hiyo nyota huyo wa kabumbu alitangaza
kwamba mshahara wake wote atautoa kwa mashirika ya kutoa msaada.
Beckham alijunga na timu ya Manchester United akiwa na umri wa
miaka 14 na kufaulu kuichezea klabu hiyo mechi 398 huku akishinda mataji sita
ya Premier League na kombe la klabu bingwa barani Ulaya. Nyota huyo Muingereza
amesema kuwa anaishukuru sana timu ya PSG kwa kumpa fursa ya kuendelea kucheza
lakini anahisi kuwa huu ni wakati mzuri kwake kumaliza kazi yake ya kucheza
mpira. Pamoja na PSG kubeba kombe la Ligue 1 la Ufaransa, katika uchezaji wake
Beckham amezoa jumla ya mataji 19 - 10 kati yao yakiwa ni mataji ya ligi kuu
mbali mbali ulimwenguni. Bechkam ndie mchezaji wa kwanza wa Uingereza kuwahi
kubeba makombe ya ubingwa wa Ulaya akichezea timu katika nchi nne tofauti.
DW.