Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw amewaita kikosini wachezaji wane wapya kwa mechi za kirafiki za Ujerumani dhidi ya Ecuador na Marekani, huku nyota wa Bayern Munich na Borussia Dortmund wakiwachwa nje kwa sababu ya fainali ya Champions League.
Wachezaji wa Real Madrid Mesut Oezil na Sami Khedira pia
watakosa ziara hiyo kwa sababu msimu wa Ligi ya Uhispania hautakuwa
umekamilika. Jumla ya wachezaji 15 wa kikosi cha kwanza hajawajumuishwa katika
ziara hiyo ya Marekani. Ujerumani itamenyana na Ecuador Mei 29 mjini Boca Raton
na kasha Marekani mnamo Juni 2 mjini Washington DC.
Mshambulizi wa Lazio Miroslav Klose na wachezaji wawili wa
Borussia Dortmund, Kevin Grosskreutz and Sven Bender, wanatarajiwa kujiunga na
kikosi cha taifa baada ya kumaliza majukumu ya klabu yao, kwa mechi ya kirafiki
dhidi ya Marekani. Wachezaji wapya walioitwa kikosini ni beki Philipp
Wollscheid wa Nuremberg, viungo Sidney Sam wa Bayer Leverkusen, Nicolai Mueller
wa Mainz na Max Kruse wa Freiburg. Wengine walioitwa ni viungo Aaron Hunt
(Werder Bremen) na Stefan Reinartz (Bayer Leverkusen).pamoja na mabeki Dennis
Aogo (Hamburger SV) na Andreas Beck (Hoffenheim).