Friday, May 17

Dortimund yaitahadharisha Bayern Munich

Zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya Fainali ya kukata na shoka ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Wembley jijini London, mengi yanaendelea kufanywa ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya dimba hilo.
Mkufunzi wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp amesema ana matumaini kwamba timu yake inaweza kuizidi nguvu Bayern Munich na kumaliza safari yao ya kujiondoa kutoka maisha ya kufilisika iliyoanza mwaka wa 2005.
Dortmund watapambana na Bayern katika uwanja wa Wembley mnamo Mei 25 kwa ubingwa huo wa Ulaya, ikiwa ni miaka minane baada ya kuomba mkopo wa euro milioni mbili kutoka kwa mahasimu wao hao Bayern ili kuwalipa mishahara wachezaji.
Klopp anasema kama watashinda, hawatakuwa timu bora ulimwenguni, lakini watakuwa wameipiku timu bora ulimwenguni kwa sasa. Hata hivyo amekiri kuwa mabingwa hao wa msimu huu wa Bundesliga Bayern, wanastahili kupigiwa upatu katika kile kitakachokuwa ni Fainali ya kwanza kuwahi kuchezwa na vilabu viwili vya Ujerumani. Na bila shaka Kansela Angela Merkel amedhibitisha kuwa atahudhuria fainali hiyo katika uwanja wa Wembley ili kuwa sehemu ya historia. Ijapokuwa amekataa kuitaja timu atakayoishabikia kati ya hizo mbili.
DW.