Tuesday, May 28

Kongo yagawika pendekezo la Kikwete

Pendekezo la Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo izungumze na makundi ya waasi na nchi jirani kutatua mzozo wa mashariki ya nchi hiyo linaonekana kuwagawa Wakongo.
Kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, kuna mwangwi wa sauti za Wakongomani wakiupongeza msimamo wa Rais Kikwete kwamba kuweko na mtazamo wa ujumla katika kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa kanda ya Maziwa Makuu.
Mwandishi wetu wa Kinshasa anaripoti kwamba wakaazi wengi wa mji huo wanaamini kuwa pendekezo hilo la Rais Kikwete linaweza kusaidia amani ya kudumu.
Kwenye mkutano wa marais 11 wa Nchi za Maziwa Makuu kwa ajili ya Kongo uliotishwa kando ya mkutano wa Umoja wa Afrika, mjini AddisAbaba, Rais Kikwete alipendekeza kufanyike mazungumzo baina ya Kongo na kundi la waasi la M23, Rwanda na kundi la waasi la FDLR na Uganda na waasi wake wa ADF/Nalu kwa ajili ya amani ya kudumu ya kanda ya Maziwa Makuu.
Tanzania inachangia wanajeshi 1,280 kwenye kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Kongo,
Umoja usio wa kawaida Kinshasa
Pendekezo hili limezua kile mwandishi wetu wa Kinshasa anachokiita “tukio la nadra kabisa nchini Kongo“ kwa wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala kuwa na kauli moja kuhusu maswala muhimu ya kitaifa.
Rais Kikwete amefanikiwa kuwaelekeza wanasiasa wa Kongo kuchukuwa msimamo wa pamoja kuhusu juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu kwenye kanda ya Maziwa Makuu.
Kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya habari ni kwamba Rais Kikwete aliwambia maraisi wenzake pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Afrika, kwamba ni lazima kuweko na mtizamo wa ujumla kwa ajili ya kumalizisha machafuko ya miaka mingi kwenye kanda la Maziwa Makuu.
Kwa hiyo Rais Kikwete alipendekeza Kongo kuendesha mazungumzo na waasi wa M23, na vilevile kuitaka Rwanda kuzungumza na waasi wa FDLR na Uganda kufungua mazungumzo na waasi wake wa ADF/Nalu. Pendekezo hilo limepongezwa na upinzani na chama tawala nchini Kongo, akiwemo mbunge Justin Bitakwira, ambaye ni kiongozi wa wabunge wa upinzani wa UNC.
Naye Franklin Tshamala, msemaji wa muungano wa vyama tawala, amesema kwamba pendekezo hilo la Rais Kikwete ni hatua ya ujasiri ya kutaka kurekebisha mitizamo tofauti waliyonayo viongozi wa mataifa haya matatu.
Rwanda yakataa
Pendekezo hilo la Rais wa Tanzania lilipongezwa pia na serikali ya Kongo. Akiwa mjini Addis Ababa, Waziri wa Mambo ya Nje ya Kongo, Raymond Tshibanda, aliiambia Radio France Internationale kwamba msimamo huo unalingana na ombi la miaka mingi la serikali ya Kongo kwa majirani zake.
Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, aliyehojiwa na redio hiyo hiyo alisema matamshi hayo ya Rais Kikwete ni ya upotofu na nchi yake haiwezi kamwe kuzungumza na watu waliohusika na mauwaji ya halaiki.
Magazeti mengi ya siku ya Jumanne (tarehe 28 Mei) yamezungumzia matamshi ya Rais Kikwete na maoni ya wananchi wa Kongo. Gazeti Lavenir limechapisha kichwa cha habari kwa wino mzito kikimuita Rais Kikwete ”Jjasiri wa kanda ya Maziwa Makuu.”
Kwenye ukarasa wa mwanzo, gazeti la upinzani la Tempetes des Tropiques limeandika “Kikwete arusha bomu Addis Abeba”, likiyaelezea matamshi ya Rais Kikwete kuwa sawa na bomu alilowarushia marais wenzake ambao kwa muda mrefu wameonyesha unafiki katika kumaliza machafuko ya Maziwa Makuu kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Goma hawataki mazungumzo na M23
Lakini hali ikiwa hivyo mjini Kinshasa, kwenye eneo la mashariki ya Kongo, ambako ndiko hasa kwenye mgogoro kati ya serikali na waasi wa M23, maoni ni tafauti.
Mwandishi wetu wa Goma, John Kanyunyu, anaripoti kwamba mashirika ya kiraia ya huko yamekataa mazungumzo baina ya serikali ya DRC na wajumbe wa M23.

Makamu mwenyekiti wa mashirika ya hayo kiraia katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, ambaye pia ni msemaji wa mashirika hayo, Omar Kavota, amesema “hakuna tena la kuzungumza, kwani tayari mkataba wa M23 baina ya chama cha zamani cha uasi CNDP umeshajadiliwa.”

Kauli hiyo ya mashirika ya kiraia inakuja baada ya pendekezo la Rais Kikwete mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na marais wa kanda ya Maziwa Makuu kuiomba serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo baina yake na waasi wa M23.
Aidha kauli hiyo ya mashirika ya kiraia ya kuitaka serikali kutozungumza na wajumbe wa M23, inachochewa pia na utendaji kazi wa wanajeshi wa serikali katika uwanja wa mapigano.

Katika vita baina ya jeshi la serikali, FARDC, na waasi wa M23, jeshi hilo la serikali linatajwa kuwa, lilifaulu kwa mara ya kwanza kabisa, kuwazuia waasi wa M23 kuuteka upya mji wa Goma.

Kavota anasema ni bora zaidi kuwapatia nafasi ya kufanya kazi zao wanajeshi wa kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kinachowajumuisha wanajeshi kutoka Tanzania, Malawi na Afrika ya Kusini.
Katika kuwapongeza wanajeshi wa serikali kwa kazi waliyoifanya wakati wa mapigano ya wiki iliyopita, mashirika ya wanawake kutoka asasi za kiraia na vyama vya kisiasa, wametoa mchango wa pesa wa kile walichokiita “kuwanunulia wanajeshi wa serikali maji ya kunywa.”
DW - SWAHILI.