Malkia Beatrix , mwenye haiba ya kupendwa na wengi amemaliza utawala wake wa miaka 33 leo, katika sherehe iliyotangazwa moja kwa moja na Televisheni na utiaji saini wa kumkabidhi Ufalme mwanawe wa kiume kushuhudiwa na maelfu ya Waholanzi waliovalia sare za rangi ya machungwa. Pia sherehe hiyo imeshuhudiwa na mamilioni ya watazamaji kwa njia ya Televisheni.
Kutokana na kuuacha Umalkia, Beatrix sasa anakuwa Princess Beatrix na mwanawe anakuwa Mfalme Willem Alexander, mfalme wa kwanza wa Uholanzi tangu alipofariki Willem wa tatu 1890.
Mfalme Willem Alexander na familia yake
Mfalme Willem-Alexander mwenye umri wa miaka 46, mkewe mzaliwa
wa Argentina Malkia Maxima na watoto wao watatu wakike walihudhuria
sherehe hiyo ya leo. Binti yao wa kwanza Catharina-Amalia mwenye umri wa
miaka 9 ndiye mrithi wa kwanza wa kiti baada ya baba yake. Wengine ni
Alexia mwenye umri wa miaka 7 na Ariane miaka 5.Malkia Beatrix mwenye umtri wa miaka 75, alitamka " Mimi Malkia Beatrix ninaacha kiti changu na kumkabidhi mwanangu wa kiume Willem-Alexander'' na mara baada ya wote wawili kusaini waraka wa kukabidhiana madaraka Mfalme huyo aliyeonekana kujaa hisia , alimkamata mkono mama yake.
Familia kadhaa za Kifalme kutoka sehemu mbali mbali duniani zilihudhuria sherehe hiyo, akiwemo mwana mfalme Charles wa Uingereza, Mwana mfalme Filipe wa Uhispania na mkewe na Mwana mfalme Naruhito wa Japan na mkewe Masako
Ilikuwa shamra shamra kwa wakazi wa Amsterdam
Leo familia ya Kifalme itakuwa na sherehe kwenye meli moja
itakayozunguka eneo la maji katika jiji la Amsterdam. Ulinzi kwa jumla
ulikuwa mkali kukiwa na polisi wapatao 10,000, askari kanzu 3,000 pamoja
na watumishi wa kiraia waliosaidia kufanikisha hafla hiyo.Umaarufu wa Willem-Alexander, uliongezeka baada ya kusema katika mahojiano hivi karibuni kwamba anataka kuwa Mfalme wa jadi wa karne ya 21, lakini hatokuwa mtu wa itifaki.
Wachambuzi wanamtaja Mfalme mpya kuwa mtu aliyebadilika mno, kutoka maisha ya ujana na starehe na kuwa mtu wa familia anayependwa na watu wake. Kitaaluma Mfalme Willem-Alexander ana leseni ya urubani zikiwemo ndege za biashara. Alikuwa rubani wa Shirika la ndege la Uholanzi KLM.
Mtindo wa kimaisha wa ufalme huo kwa upande mwengine, haukuepuka kushutumiwa.
Mwezi Novemba mwaka 2009, Willem Alexander aliuza jumba lake la kifahari alilokuwa akijenga kwenye mwambao wa Msumbiji, kutokana na shinikizo la maoni ya umma, ambayo yalilichukulia jumba hilo kama mali ya anasa katika sehemu ya Afrika inayozongwa na umasikini mkubwa.
DW - SWAHILI.