Mabingwa wa kombe la dunia Uhispania watachuana na Brazil katika fainali ya kombe la Shirikisho siku ya Jumapili baada ya kuishinda Italia katika mechi ya nusu fainali kupitia kwa mikwaju ya penalti.
Uhispania ilijikatia tikiti ya fainali hiyo kwa kuilaza Italia kwa magoli saba kwa sita mjini Fortaleza.
Mchezaji wa akiba Jesus Navas, ndiye aliyeifungia Uhispania bao lake la ushindi baada ya mlinda lango wa Italia Leonardo Bonucci kupoteza zamu yake.
Katika dakika tisini za kawaida, Italia ilionekana kutawala mechi hiyo, lakini juhudi zao ka kufunga ziliambulia patupu.
Katika muda wa ziada mkwaju wa Emanuele Giaccherini, uligonga mlingoti wa goli la Uhispania naye Gianluigi Buffon alizuia mkwaju wa Xavi Alonzo na kuifanya ugonge pia mlingoti wa goli.
Navas ambaye anajiunga na Manchester City msimu ujao alifunga bao la mwisho na kuhakikisha kuwa mabingwa hao wa dunia wanachuana na wenyeji wa mashindano hayo Brazil ambao walishinda mechi yao ya nusu fainali dhidi ya Uruguay kwa magoli mawili kwa moja siku ya Jumatano.
Italia sasa itachuana na Uruguay kutafuta mshinda wa tatu na nne siku hiyo hiyo ya Jumapili.