Pazia lashuka katika michuano ya kombe la mabara nchini Brazil, mabingwa wa Ulaya na dunia Uhispania waonja " joto ya jiwe" , Brazil yaibuka kidedea.
Je kipigo cha jana(30.06.2013) cha mabao 3-0 ilichokumbana nacho mabingwa wa dunia na Ulaya Uhispania dhidi ya Brazil katika fainali ya kombe la mabara, Confederations Cup , ni kwikwi tu ama inatoa ishara ya mwisho wa enzi za tiki taka ya kikosi hicho cha La Roja?.
Hilo ndio swali ambalo vyombo vya habari vya Uhispania na wadadisi wengine wa masuala ya soka duniani walikuwa wanajiuliza leo, baada ya kipigo cha kudhalilisha katika mchezo wa kwanza wa mashindano kwa Uhispania tangu mwaka 2010.
Vyombo vingi vya habari za michezo vimejaribu kuangalia kadhia hiyo iliyowapata Uhispani kuwa ni bahati mbaya tu katika siku mbaya kwa kocha Vicente del Bosque na kikosi chake.
Kwa mfano kichwa cha habari katika gazeti maarufu la Marca kinasema , "Tutarejea", wakiashiria fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil.
Del Bosque akiri
Del Bosque binafsi ameweka msisitizo katika matamshi kama hayo kwa kusema , "mara nyingine ni vizuri kushindwa, tumekuwa hatuna bahati kwa kufungwa mabao katika wakati muhimu. Goli la kwanza lilikuwa muhimu lakini hiyo haiwezi kuwa sababu iliyosababisha tufungwe.
Walicheza mchezo wa kuweka mbinyo dhidi ya timu yetu na kuvunja mtiririko wa mchezo wetu kwa kufanya rafu nyingi. Hata hivyo kocha huyo mzoefu , ambaye ameiongoza uhispania kupata ushindi katika kombe la dunia mwaka 2010 na Euro 2012, alikuwa mwepesi pia kuwapongeza Brazil. ilikuwa timu nzuri sana dhidi yetu ni mabingwa wanaostahili. Amesema Del Bosque.
Brazil inashauku kubwa wakati inajiwinda kuingia katika fainali za kombe la dunia mwaka 2014 nchini humo kwa mtazamo tofauti baada ya pazia kushuka katika kinyang'anyiro cha kombe la mabara jana.
Confederations Cup imeelezwa na rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Joseph Sepp Blatter kuwa ilikuwa ni tamasha murua kabisa.
Hata hivyo mashindano hayo yaliyojumuisha timu nane yaliyofanyika katika viwanja sita kati ya 12 ambavyo vitatumika kwa fainali za kombe la dunia yamefanyika huku kukiwa na maandamano tangu mwanzo hadi siku ya mwisho nchi nzima.
Polisi wakuzuwia ghasia walitanda , na ghasia ziliendelea mjini Rio de Janeiro karibu na uwanja uliofanyika fainali hiyo wa Maracana.
Neymar nyota inayong'ara
Lakini nyota anayechipukia wa Brazil Neymar alijitokeza kuwa mmoja wa vijana watakaoweza kuichukua Brazil katika kiwango cha juu katika medani ya soka ya dunia. Alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo, alipachika wavuni mabao manne na kutoa pasi kadha za kufunga mabao kwa wenzake, na huenda muhimu zaidi amekuwa kiongozi muhimu katika kikosi cha timu ya Brazil cha 'Verdeamarela'.
Wachezaji wa Uhispania pia walifurahishwa na mchezaji huyo, kama anavyosema mlinzi wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania Gerard Pique ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu zikiwa zimesalia dakika 20 kabla ya mchezo wa fainali kumalizika , kwa kumwangusha Neymar ambaye atakuwa mchezaji wa timu yake ya Barcelona , karibu na eneo la hatari.
"Ni hodari sana. Ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu kabisa, ni mwepesi wa kwenda kasi , ameonesha hali hiyo muda wote wa mashindano. Na zaidi ya hayo anafunga magoli. ninafurahi sana kwa kuwa atakuwa upande wetu mwaka ujao na Barcelona."
naye mwenyewe Neymar kuhusu ushindi wa Brazil amesema ulikuwa muhimu sana.
"Leo ndoto yangu imekuwa kweli. Nina furaha sana. Na ulikuwa mchezo mzuri na tumenyakua taji hili."
Mshambuliaji wa Brazil Fred ambaye alipachika mabao mawili usiku wa jana aliuelezea ushindi huo kuwa ni mtamu sana kwao.
"Ulikuwa ni ushindi mnono , ukitilia maanani hisia za pamoja za wachezaji wetu na kazi tuliyokuwa tukiifanya kwa muda mrefu pamoja na kocha Felipe Scolari. Katika wakati fulani , kulikuwa na ukosefu wa kujiamini baina ya wachezaji na wafanyakazi wa timu na ukosefu wa kujiamini kwa nje, lakini tumeweza kuwavuta mashabiki upande wetu."