Taarifa kutoka ofisi ya rais wa Misri Mohammed Morsi imesema kuwa rais huyo atashikilia mpango wake wa kuleta maridhiano ya kitaifa ili kutatua mzozo wa kisiasa unaokabili taifa hilo.
Hilo ndilo tamko la kwanza kutoka kwa rais huyo tangu jeshi litoe makataa ya saa arobaini na nane kuwataka wanasiasa kutoka pande zote kutatua mgogoro huo.
Taarifa hiyo ya rais imesema kuwa hatua hiyo ya jeshi kuingilia kati itazua hali ya suitofahamu zaidi.
Jeshi limetoa makataa ya saa arobaini na nane kwa Morsi kutatua mgogoro wa kisiasa unaokumba taifa hilo la sivyo watachukua hatua.
Jeshi limekanusha madai kuwa makataa hayo ni sawa mapinduzi ya kijeshi.
Serikali imesema kuwa Morsi amewasiliana na rais Barack Obama kuhusu hali ya kisiasa inayoshuhudiwa Misri.
Wakati huohuo, shirika la habari la kitaifa Misri, limeripoti kuwa waziri wa mambo ya nje Mohamed Kamel Amr amejiuzulu.
Ikiwa ombi lake litakubaliwa, atakuwa mmoja wa mawaziri wengine watatno ambao wamejiuzulu kufuatia mgogoro huo wa kisiasa.
Mnamo jumapili, mamilioni walifanya maandamano wakimtaka rais ajiuzulu.
Maandamano mengine makubwa yalishuhudiwa Jumatu huku ripoti zikisema kuwa watu wanane waliuawa wakati waandamananaji walipovamia makao makuu ya chama tawala cha Muslim Brotherhood.
Wapinzani wa Morsi,wanamkosoa kwa kuweka maslahi ya chama mbele huku akiwapuuza wale wasiounga chama hicho.
Morsi alichaguliwa kama rais wa kwanza wa kiisilamu katika uchaguzi wa mwezi Juni mwaka 2012 tarehe 30 bbaada ya kushinda uchaguzi uliotazamiwa na wengi kuwa huru na wa haki baada ya mapinduzi ya kiraia yaliyomwondoa mamlakani Hosni Mubarak.