Kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na kuzidi kwa kiwango cha sukari mwilini, kunakoweza kusababishwa na ulaji mwingi wa sukari au kushindwa kwa kongosho (pancrease) kuzalisha kichocheo cha insulin ambacho ndiyo hufanya kazi ya kurekebisha kiwango cha sukari kwenye damu.
Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yanayowatesa watu wengi duniani, huku ukielezwa kusababisha vifo vingi.
Aina za Kisukari
Ugonjwa huu wa kisukari, kitaalam umegawanyika katika makundi makuu matatu
1. Type 1 Diabetes Melitus (Juvenile)
Aina hii husababishwa na mwili hususan kongosho kushindwa kuzalisha insulin inayoratibu kiwango cha sukari mwilini.
2. Type 2 Diabetic Melitus (Adult)
Aina hii husababishwa na seli za mwili kushindwa kusanisi insulin ambayo tayari imeshazalishwa na kongosho na kuingizwa kwenye damu.
3. Gestational Diabetes
Aina hii ya ugonjwa huwapata akina mama wajawazito ambao hawakuwahi kuwa na tatizo hilo lakini kiwango cha damu kwenye miili yao kinaongezeka ghafla baada ya kushika ujauzito.
Aina nyingine za ugonjwa wa kisukari ni Congenital Diabetes ambayo hurithishwa, Steroid Diabetes, Monogenic Diabetes na nyingine nyingi.
Habari njema kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na kisukari ni kwamba ugonjwa huo hivi sasa unatibika na wapo watu waliothibitishwa kupona kabisa. Hata hivyo, wagonjwa wasipowahishwa hospitali, hupatwa na matatizo mengine kama hypoglycemia, diabetic ketoacidosis na hyperosmolar coma. Pia husababisha matatizo ya moyo na mwisho husababisha kifo.
Dalili za awali za kisukari ni kupungua uzito, kukojoa mara kwa mara (polyuria), kuhisi kiu mara kwa mara (polydipsia) na kuhisi njaa kali mara kwa mara (polyphagia).
Dalili nyingine ni macho kupoteza uwezo wa kuona kunakosababishwa na kubadilika kwa muundo wa lenzi za macho, maradhi ya ngozi (dermadromes), matatizo katika mfumo wa upumuaji, kuhisi kichefuchefu na kutapika mara kwa mara, maumivu ya tumbo chini ya kitovu na kukosa umakini na uzingativu.
Dalili nyingine ni kuharibika kwa mishipa ya damu ndani ya mwili, kukojoa mkojo wenye kiwango kikubwa cha sukari au protini, mwili kufa ganzi, kuvimba miguu na dalili nyingine nyingi.
CHANZO CHA KISUKARI
Kama ilivyoelezwa awali, sababu kubwa za ugonjwa huu ni kongosho kushindwa kuzalisha insulin ambayo ndiyo hurekebisha kiwango cha sukari mwilini. Sababu nyingine ni:
-Mitindo ya maisha
Ulaji wa vyakula vyenye sukari na mafuta kwa wingi, inatajwa kuwa sababu kubwa ya ugonjwa wa kisukari.
-Maambukizi ya virusi vya Coxsackie B4 virus
Virusi hivi vinatajwa kusababisha ugonjwa wa kisukari ingawa ni kwa kiasi kidogo. Vikiingia mwilini, huenda kushambulia seli za Islet of Lengerhans kwenye kongosho.