Ugonjwa wa Saratani bado ni tishio Tanzania
Wakati walimwengu wakiadhimisha Siku ya Saratani leo, ugonjwa huo nchini Tanzania umeelezwa kukua kwa kasi, huku waathirika wa tatizo hilo wakiwa ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 25 na 30. Daktari wa Kitengo cha Patholojia cha Uchunguzi wa Magonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam Innocent Mosha amesema, kati ya wagonjwa 17 na 20 hugundulika na saratani kila siku katika hospitali hiyo ya taifa.
Ameongeza kuwa, kwa mwaka wagonjwa wanaogundulika kuwa na saratani Muhimbili ni zaidi ya 4,000. Amesema, takwimu hizo ni za Hospitali ya Taifa Muhimbili tu, bado kuna Ocean Road, mikoani na hospitali nyingine binafsi. Daktari Bingwa wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa wa Muhimbili mjini Dar es Salaam Tanzania, Henry Mwakyoma amesema kuwa, saratani kuu zinazoongoza nchini humo ni pamoja na saratani ya shingo ya kizazi, tezi dume, ngozi, mifupa, tezi kwa watoto na wakubwa, damu, kongosho, ubongo na ini.