Tuesday, July 16

Fabregas asema hataki kurudi England

Mcheza kiungo wa Barcelona Cesc Fabregas amesema hana nia yoyote ya kuihama klabu hiyo na kurejea tena nchini England.
Hayo ni kwa mujibu wa kocha wake Tito Vilanova.
Klabu ya Manchester United siku ya Jumatatu iliwasilisha ombi la kutaka kumasajili nahodha huyo wa zamani wa Arsenal, kwa kitita cha pauni milioni ishirini na tano, lakini Vilanova amesema mchezaji huyo anataka kusalia nchini Uhispania kwa sasa.
''Ni ishara nzuri kwa klabu yoyote kupata maombi kutoka kwa vilabu vingine, vinavyotaka kuwasajili wachezaji wake, lakini Fabregas amesema anataka kusalia'' Alisema kocha huyo.
Vilanova ameongeza kusema kuwa'' Fabregas hataki kujiunga na timu zingine kwa sababu ya pesa au kutokana na muda wake wa kucheza uliosalia. Anafahamu huku kuna ushindani mkali, lakini ni uamuzi wake kusalia na Barcelona. Kwa sasa nimetulia''.
Kufikia sasa Barcelona halijasema lolote rasmi kuhusiana na ombi hilo la Manchester United, ambalo linaaminika kuwa chini ya dhamana kamili ya mchezaji huyo.
Fabregas alikuwa mchezaji mchanga zaidi wa Arsenal wakakti aliocheza dhidi ya Rotherham United wakati wa mechi ya kombe la ligi mwaka wa 2003 akiwa na miaka kumi na saba na siku mia moja na sabini na saba.
Alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Arsenal walioishinda timu ya Manchester United kupitia mikwaju ya penalti kwa fainali ya kombe la FA mwaka wa 2005.
Vile vile Fabregas, anaichezea timu ya taifa ya Uhispania na aliisaidia kunyakua kombe la dunia na pia kuwa mabingwa wa bara Ulaya mara mbili.
Alijiunga na Arsenal mwaka wa 2003 akiwa na umri wa miaka kumi na sita.
Fabregas aliichezea Arsenal mechi 303 na kufunga magoli 57, kabla ya kusajiliwa na Barcelona kwa kitita cha pauni milioni 25.4 kwa mkataba wa miaka mitano kwa wa 2011.

BBC