Wednesday, July 17

Serikali yatenga bil. 30 kwa tafiti za kisayansi.

Serikali  imewekeza Sh.bilioni 30 kwa ajili ya utafiti wa kisayansi kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari hususani wale wanaosomea masomo hayo.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa wakati wa kukabidhi zawadi kwa wanafunzi wa shule zilizoshinda shindano la kutafuta wanasayansi chipukizi toka shule 100 nchini.
“Bila kuwekeza katika utafiti wa kisayansi, nchi haiwezi kuendelea…hivyo kama serikali tumeamua kutenga kiasi hicho kwa lengo la kufanyia tafiti mbalimbali kuanzia kwa wanafunzi hawa toka shule mbalimbali hapa nchini,” alisema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa alisema serikali itaboresha utafiti huo ili kuwapa nafasi wanafunzi wengi kuwa wagunduzi wa mambo ya kisayansi kutokana na sayansi kutokuwa na mipaka.
Alisema ili kuendeleza sayansi nchini, serikali imejenga chuo kikubwa kiitwacho Nelson Mandela jijini Arusha na kutarajiwa kuzinduliwa Novemba 2, mwaka huu, chenye lengo la kuendeleza utafiti wa sayansi.
Aidha, alisema katika mashindano ya wanasayansi chipukizi toka shule mbalimbali za sekondari nchini, serikali itawasaidia waandaji wake, Young Scientists Tanzania  (YST), kuwezesha wanafunzi zaidi kushiriki tofauti na sasa ambapo shule 100 zenye wanafunzi 300 hushiriki.
“Taasisi nyingi nazo za tafiti za kisayansi zinatakiwa kushiriki maonyesho kama haya siku zijazo…lengo letu likiwa ni kuwekeza katika sayansi nchini,” alisema.
Awali mkurugenzi wa YST, Gosbert Kamugisha alisema lengo la mashindano hayo kwa wanasayansi chipukizi toka shule mbalimbali za sekondari nchini, ni kulenga tafiti za kisayansi.
“Wanafunzi walitakiwa kuandika maombi ya kisayansi yenye kulenga tafiti za kisayansi…tumeshirikisha wanafunzi 300 toka shule 100 za Bara na Visiwani, na washindi wametangazwa na kupewa zawadi zao,” alisema Kamugisha.
Alisema katika mashindano hayo watafiti wa kisayansi toka Chuo cha Taifa cha Ireland, walikuwa wakitoa muongozo.
Katika mashindano hayo, shule ya wasichana ya Kibosho ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza na kujishindia nishani, Sh.Milioni moja pamoja na kompyuta mpakato (Laptop) tatu.
Wizara ilitoa Laptop hizo kwa wanafunzi watatu wa shule hiyo wanaosoma kidato cha tano waliofanya vizuri ambao ni Monica Shirika na Nengai Moses wanaochukua mchepuo wa PCB pamoja na Aisha Nduka wa mchepuo wa PCM, huku shule ya Ilboro Arusha ikikabidhiwa Sh.Milioni Moja kwa ushindi wa pili.

TANZGLO