Raisi wa jamhuri ya muungano was Tanzania. |
amewatoa hofu Watanzania akiwataka walale usingizi kwa kuwa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wowote lipo tayari kulinda
nchi kwa gharama yoyote.
Aidha, amesema Serikali haitakubali hata mara moja, mtu aichezee amani
ya Tanzania na Dola iko tayari kuilinda na kuitetea nchi na akaonya
tena, kwamba hakuna atakayejaribu kuvuruga nchi, apone.
Kikwete alisema hayo jana katika kambi ya Kaboya, wilayani Muleba,
Kagera wakati akihutubia wananchi kwenye maadhimisho ya kitaifa ya Siku
ya Mashujaa na kutangazwa moja kwa moja na televisheni ya Taifa (TBC).
Maadhimisho hayo ni kumbukumbu ya wanajeshi waliokufa katika Vita ya
Kagera mwishoni mwa miaka ya sabini baada ya majeshi ya Nduli Iddi Amini
wa Uganda kuvamia nchi na kuchukua sehemu ya ardhi ya Tanzania.
Akisisitiza alichozungumza Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange
alipomkaribisha kusalimu wananchi katika sherehe hizo kuwa Jeshi lipo
imara saa 24 kulinda wananchi, Rais Kikwete alitaka Watanzania wasiwe na
hofu.
“Hamhitaji kauli zaidi ya hii (ya Mwamunyange), laleni usingizi,
msisikilize maneno ya mitaani, Jeshi liko salama na imara,
atakayejaribu, atakiona cha mtema kuni...Jeshi wakati wowote, saa
yoyote, tupo tayari kuilinda nchi yetu,” alisema Kikwete na kuongeza.
“Tutailinda, tutaitetea, hatutakubali mtu aichezee, hatuna nchi
nyingine, ni hii hii, hakuna atakayepona anayetaka kuchezea nchi yetu”.
Akizungumzia kuhusu kuenzi mashujaa waliobaki waliopigana vita, Rais
Kikwete alisema ingawa hakuna uwezo wa kuwaridhisha kwa namna ya
mahitaji yao, Serikali kamwe haitaacha wateseke, itaendelea kuwaenzi kwa
kuwa walijitoa muhanga kwa nchi yao.
“Wenzetu walijitoa muhanga kwa ajili yetu, kuhakikisha usalama wa nchi
kuna gharama zake, Taifa haliwezi kuwasahau, Serikali itaendelea
kuwajali, wapo mashujaa wenzetu waliokwenda Msumbiji, baadhi nao
wamelala, waliobaki tutaendelea kuwajali,” alisisitiza Kikwete.
Aligusia ukaidi wa Amini na majeshi yake alipovamia nchi mwaka 1978,
akisema baada ya kuingia Kagera na kubadili ramani na kudai Mto Kagera
ndio mpaka, aliharibu mali nyingi na Amiri Jeshi Mkuu wakati huo,
Mwalimu Julius Nyerere alimwamuru aondoke akakataa, ndipo akavamiwa na
kushindwa vibaya.
“Ili kumwonesha kuwa uwezo tunao, Mwalimu Nyerere aliamuru pamoja na
kumtoa katika ardhi yetu, aondoke kabisa madarakani na pia majeshi yetu
yaliingia Uganda eneo la Masaka na Mbarara kushambulia ili wapate
uchungu wa kujenga kama waliotupatia sisi,” alifafanua Rais Kikwete
akidhihirisha kwa mifano, uwezo wa Jeshi la Tanzania.
Rais Kikwete awali pamoja na kumkaribisha Jenerali Mwamunyange kusalimia
wananchi, pia alikaribisha viongozi wengine wa ngazi za juu
waliohudhuria sherehe hizo kuwasalimia wananchi akiwamo Makamu wa Rais
wa Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein na ambao wote walisisitiza kuilinda amani ya nchi.
Wengine waliohudhuria na kusalimu wananchi ni pamoja na Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman
Makungu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo pia kutaka wabunge wa majimbo mawili
ya Muleba, Charles Mwijage wa Kaskazini na Profesa Anna Tibaijuka wa
Kusini, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kueleza matatizo yanayokabili wananchi wa eneo hilo.
Mwijage (CCM) alisema miongoni mwa changamoto kubwa katika eneo hilo ni
utata wa mpaka wa kambi hiyo ya Jeshi ya Kaboya kutojulikana na
kusababisha uhusiano mbaya kati ya wakazi wa eneo hilo na Jeshi, kwa
kuwa wanashindwa kujua walime mpaka wapi.
Mbunge huyo alisema pia kuwa ujenzi wa madaraja mawili likiwamo la
Kishala na mradi wa kuvua samaki ambao Serikali iliwezesha mtu kwenda
kujifunza Vietnam na China, ni mambo yanayowatatiza wananchi wa jimbo hilo.
Akijibu changamoto hizo, Kikwete alitaka watendaji wa wilaya na mamlaka
husika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa na kuwambia wakikwama
wamweleze, kwa kuwa yeye ndiye mtoa fedha za miradi ya wananchi.
Kuhusu umeme vijijini, Kikwete alisema umeme utafika ulikoahidiwa,
alimwita Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe kuwaeleza wananchi
ulikofikia na Massawe alisema tayari umeanza katika vijiji kadhaa na
Muleba utafika kama ulivyoahidiwa kupitia Wakala wa Umeme Vijijini