Urithi wa Dunia ni maeneo yenye thamani kubwa ya kiutamaduni au kimazingira duniani yanayoangaliwa na shirika la UNESCO.
Hadi mwisho wa mwaka 2009 sehemu 890 katika nchi 148 zimekubaliwa. Nchi inayoongoza kwa wingi wa mahali ni Italia yenye 45.
Orodha rasmi ya UNESCO ina mahali 689 pa urithi wa dunia wa kiutamaduni na mahali 176 pa urithi wa dunia wa kimazingira, mbali ya 25 pa mseto.
Mwanzo wa jitihada za kuhifadhi urithi wa dunia ulikuwa ujenzi wa bwawa la Assuan lililoelekea kuzamisha majengo mbalimbali ya utamaduni wa Misri na Nubia wa kale chini ya maji. Wakati ule UNESCO ilifaulu kukusanya pesa ilihekalu la Abu Simbel liweze kuhamishwa mlimani kabla ya kujaa kwa bwawa.
Tangu 1972 kuna mkataba wa kimataifa wa Stockholm kuhusu hifadhi ya urithi wa dunia kiutamaduni na kimazingira.
Kila mahali panapopendekezwa ili pakubaliwe panahitaji angalau sifa moja kati ya sita zifuatazo:
- kuwa na thamani ya pekee ya kisanii
- kuwa na athira muhimu katika eneo fulani au kipindi cha historia
- kuwa kitu cha pekee kisichopatikana tena au kuwa na umri mkubwa
- kuwa mfano bora wa kipindi fulani cha historia ya ujenzi
- kuwa muhimu katika uhusiano na fikra muhimu au watu muhimu wa historia
Kamati ya Urithi wa Dunia hukutana kila mwaka na kuangalia maombi ya kupokelewa katika orodha ya urithi wa dunia. Kamati inapokea taarifa kuhusu hifadhi na hali ya urithi uliopo tayari orodhani. Kila baada ya miaka miwili orodha inatolewa upya.