Mtwara. Meli kubwa kutoka China tayari imetua katika Bandari ya
Mtwara kwa ajili ya kushusha mizigo ya mabomba ya gesi ili kuanza kwa
kazi ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es
Salaam.
Mmoja wa watumishi ndani ya Bandari ya Mtwara
ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema zaidi ya magari 20
yanatakiwa kupakua mzigo wa mabomba zaidi ya 4,000 kutoka bandarini
hapo na kusafirishwa kwenda Kiranjeranje Lindi kwa ajili ya zoezi zima
la ujenzi wa bomba hilo.
“Hayo magari mliyoyaona ni miongoni mwa zaidi ya
magari 20 yanayokuja kupakua mzigo wa mabomba ambayo ni zaidiya 4,000
kwa ajili ya kuyapeleka maeneo mbalimbali ikiwemo Kiranjeranje Lindi kwa
ajili ya kufanikisha zoezi la ujenzi wa njia ya kusafirisha gesi,
upakiaji unaendelea hapa Mtwara na Dar meli inapakuwa mzigo ili
kupelekwa kwenye maeneo husika na upakuaji kwa mikoa yote unaendelea kwa
amani,” alisema.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa madereva wa
magari maalumu kwa ajili ya kupakua mzigo wa mabomba,alisema wametokea
Dar es Salaam na hii ni zabuni maalumu waliyoipata kwa ajili ya
maandalizi ya kupokea mizigo na kupeleka yanakotakiwa hapo baadaye
baadaye baada ya kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
“Hivi sasa tunaenda kupakiza mzigo kwa ajili ya
maandalizi tukisubiri siku ambayo wahusika wakuu watakaokabidhiwa,ili na
sisi tuanze zabuni yetu ya usafirishaji kuyapeleka yanakohitajika, “
alisema
Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo Muhongo alisema tayari meli ilitua
katika bandari ya Dar es Salaam na meli kubwa imetua Mtwara kwa ajili ya
kushusha mzigo wa mabomba na watakapomaliza yatakabidhiwa na kupokewa
kwa heshima kama alivyofanya waziri mkuu jijini Dar es Salaam juzi
(Jumapili)
“ Kwa mtu anayejua uchumi kitu kitakachotutolea
umaskini ni hii gesi, mimi ninashangaa watu wa Mtwara wahoji kwa nini
mizigo mingine ishushwe Dare es Salaam badala ya Bandari yaMtwara, hata
kwa barabara wengine wanaanzia Dar na wengine wanaanzia Mtwara halafu
wanakutana, hivyo sioni sababu ya kusafirisha kwa magari baada ya
kushusha mizigo yote Mtwara ni kwa nini tuharibu barabara ?” alihoji
Profesa Muhongo.
Sudi Mohammedi alisema kitendo cha serikali kwenda
kushusha mizigo mingine katika Bandari ya Dar es Salaam ni kuonyesha ni
kwa kiasi gani viongozi wasivyoithamini Mtwara kwa kuiacha bandari
hiiyo.
Kabla ya kupita kwa magari hayo ya kubeba mizigo
maeneo ya Bima, vilianza vifaru vikifuatiwa na gari kubwa lililobeba
wanajeshi lililokuwa likizunguka katika baadhi ya maeneo mbalimbali
mkoani hapa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI