Rais mpya wa Misri ameanza kuimarisha madaraka yake na udhibiti wa mitaa hata wakati wapinzani wake wa chama cha Kiislamu wamesema kuwa mamlaka yake ni kinyume na sheria na wakidai rais Mursi arejeshwe madarakani.
Kuondolewa kwa Morsi madarakani kwa njia ya mapinduzi kumesababisha maandamano makubwa pamoja na mapambano ya mitaani kati ya makundi hasimu.
ELBaradei hatakiwi
Kuonesha hali ya mgawanyiko mkubwa unaomkabili kiongozi huyo asiye na uzoefu wa kutosha , Adly Mansour, ofisi yake imesema kuwa kiongozi anayependelea mageuzi Mohammed ElBaradei ameteuliwa kuwa waziri mkuu wa mpito lakini kauli hiyo ilibadilishwa haraka baadaye na kusema kuwa mashauriano bado yanaendelea .
Mwanasiasa ambaye yuko karibu na ElBaradei amesema hatua hiyo ya kubadilisha uamuzi inatokana na upinzani kutoka kwa chama cha kihafidhina kinachofuata siasa kali zinazoegemea dini ya Kiislamu ambacho utawala mpya unataka kushirikiana nacho.
Utawala wa Mansour , wakati huo huo , umeanza kujaribu kuondoa kile Morsi alichokijenga. Amemuondoa mkuu wa usalama wa taifa na mnadhimu mkuu wa ikulu ya nchi hiyo.
Viongozi wabaki korokoroni
Waendesha mashtaka, wakati huo huo , wameamuru viongozi wakuu wa chama cha Morsi cha udugu wa Kiislamu ambao wamewekwa kizuizini washikiliwe kwa muda wa siku 15 wakisubiri uchunguzi uendelee kuhusiana na kushambuliwa na kuuwawa kwa waandamanaji wanane wiki iliyopita.
Hakuna ghasia kubwa zilizoripotiwa kati ya waungaji mkono na wapinzani wa Morsi wakati pande hizo mbili zimejikusanya tena baada ya usiku wa mapambano makali ambayo yameufanya mji wa Cairo kuwa eneo la mapambano. Mapigano pia yamekuwa makali katika mji wa bandari wa Alexandria, ambako maelfu ya wafuasia wa kila upande walipigana kwa risasi, mabomu ya moto na virungu.
Ghasia za Ijumaa zimesababisha watu 36 kuuwawa, na kufikisha idadi ya karibu watu 75 waliouwawa tangu ghasia hizo kuzuka hapo Juni 30, wakati mamilioni ya waandamanaji wakiingia mitaani katika mkesha wa mwaka wa kwanza tangu Morsi kuingia madarakani kidemokrasia.
Morsi ambaye ni mhandisi aliyepata mafunzo yake nchini Marekani ambaye anashutumiwa sana na wakosoaji kwa kuhodhi madaraka binafsi na kwa ajili ya chama chake cha udugu wa Kiislamu pamoja na kushindwa kwake kutekeleza mageuzi ya kidemokrasia ya kiuchumi , ameendelea kubaki kizuwizini katika eneo ambalo halijilikani.
Wasi wasi wazidi
Hali ya wasiwasi imeendelea kuongezeka wakati mamia kwa maelfu ya wafuasia wa Morsi wakiingia mitaani kwa siku ya tatu karibu na msikiti katika eneo la mji wa Cairo ambalo kwa kawaida ni ngome kuu ya chama chake, wakiimba kauli mbiu za hasira dhidi ya kile wanachokiita mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na jenerali wa jeshi Abdel-Fattah el-Sissi. Jenerali huyo wa jeshi amekana kuwa amefanya mapinduzi ya jeshi, akisema kuwa alikuwa anachukua hatua za matakwa ya mamilioni ya Wamisri wanaoandamana dhidi ya rais huyo wa zamani.