Friday, March 8

Simba sc kwatikisika, viongozi wawili wajiuzuru.


Makamu mwenyekiti, Godfrey Nyange Kaburu.
Jahazi la Simba zimezidi kwenda mlama baada ya Makamu mwenyekiti, Godfrey Nyange Kaburu na Mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hans Pope kutangaza kujiuzulu rasmi nyadhifa zao jana.

Uamuzi wa kujiuzuru kwa viongozi hao unakuja wakati Simba ikiwa kwenye wakati mguu baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa kwa kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Libolo ya Angola pamoja na matokeo mabaya ya timu hiyo katika mechi zake za Ligi Kuu, raundi hii.

Sababu kubwa inayoonekana kuisababisha Simba kufanya vibaya ni pamoja na usajili mbovu ambao ulikuwa ukisimamiwa na mwenyekiti huyo aliyetumia mamilioni ya fedha kusajili wachezaji na baadaye kuwaacha.

Miongoni mwa wachezaji wa kigeni aliowasajili na
wengine kuachwa ni pamoja na Komalmbil Keita, Paschal Ochieng, Daniel Akuffo, Abel Dhaira, Emmanuel Okwi na Lino Musombo. Hivi sasa waliobaki ni Abel Dhaira na Komalmbil Keita.

Hans Pope aliyekuwa jembe la usajili la Simba amesema ameamua kuachia nafasi yake hiyo kutokana na mambo yanavyokwenda katika klabu ya Simba.

Uongozi wa Simba kupitia Katibu Mkuu, Evodius Mtawala umethibitisha kujiuzulu kwa Hans Pope ambaye amesema mambo yamekuwa hayaendi vizuri na katika mpangilio mzuri.

Mtawala alisema amepokea barua ya Hans Pope ila hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sana mpaka mpaka uongozi wa Simba utakapokutana na kujadili.

Mtawala alisema Hans Pope alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba kwa kuteuliwa, hivyo wanafanya mawasiliano na Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ambaye yupo India kwa matibabu na watakaporuhusiwa kuzungumza lolote zaidi watatoa tamko.


Kujizulu kwa Hans Pope katika klabu ya Simba ni pigo kwa Simba ambayo imekuwa ikienda kwa mwendo wa kuyumba huku matumaini yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu yakififia siku hadi siku.

Tangu kuingia kwake madarakani, Hans Pope ambaye alikuwa akitumia mamilioni ya fedha katika kusajili wachezaji Simba amejikuta akiingia katika mgogoro na uongozi wa timu hiyo pamoja na wanachama wao wakidai amefanya usajili usio na tija kwa klabu hiyo.




Lakini Hans Pope aliyekuwa msaada mkubwa ndani ya klabu hiyo katika usajili yeye alisema ameamua kuachia nafasi yake hiyo kutokana na mambo yanavyokwenda pamoja na kumaliza majukumu aliyokabidhiwa na uongozi.

Alisema ameitumikia Simba kwa muda mwingi kwa hiyo anaona ni vema akatoa nafasi kwa wengine kushika wadhifa wake kwa lengo la kuleta mabadiliko ndani ya klabu ya Simba.

"Sijashinikizwa na mtu katika uamuzi wangu, nimeamua mwenyewe baada ya kuona muda wangu wa kuitumikia Simba unamalizika kwani nataka kuwaachia na wengine, naamini kabisa majukumu niliyopewa nimeyakamilisha, kikubwa tuendelee kushikamana katika kuiendeleza timu hii,"alisema  Hans pope.

Alisema,"kama timu inafanya vibaya ni heri kuwaachia wengine wajaribu kwani lawama siyo nzuri, ni bora ufanye kitu kwa mafanikio na wanachama waridhike na mwenendo wa timu kwa hali hii sioni kama nastahili kuendelea kuingoza Simba."

Timu ya Simba inatarajiwa kuashuka dimbani mwishoni mwa juma hili kwa ajili ya kuvaana na Coastal Union ya Tanga katika mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.