Monday, July 22

Ijue Computer ( Tarakilishi ). Sehemu ya II.

Tofauti ya Data na Habari.
Data: Ni ibara ya taarifa au maelezo, na inaweza kuonekana katika sura ya maandishi, michoro, picha, namba, alama, nembo, sauti au lugha ya maandishi, au sauti pamoja na picha.
Habari (Information):
Ni kazi inayotokana na taarifa au maelezo (Data) baada ya kwisha kupangiliwa na kufanyiwa kazi kisha kutoa matokeo kamili ya kazi hiyo, pamoja na kuleta kitu chenye kufahamika na chenye faida.

Sifa za kompyuta.

Wepesi: kompyuta inafanya kazi kwa wepesi wa hali ya juu kiasi kwamba unaweza kutafuta kitu kwa muda wa sekunde chache tu, kitu ambacho kama utakitafuta kupitia chombo chengine unaweza kuchukuwa wakati mrefu mpaka kukipata na pengine usikipate, kwa mfano unaweza kufanya hesabu ngumu kwa muda mchache kuliko kutumia akili yako. Pia unaweza kutafuta somo lolote kupitia internet kwa kutumia muda mfupi kulipata somo hilo kuliko ungetumia marejeo ya vitabu vya kuchapishwa.

Ubora:Kompyuta inafanya kazi kwa ubora zaidi bila kuonyesha udhaifu na makosa ya aina yoyote, na kama itabainika ya kwamba kuna makosa yametendeka kwenye kazi yako kompyuta kabla ya kuendelea kufanya kazi inakuonyesha kwamba upo katika makosa na kukutaka mara moja kurekebisha makosa hayo kwa kukuletea tangazo lenye sehemu kadhaa za kuchagua, ima kuendelea na kazi yako kama ilivyo au kufanya marekebisho ya kazi yako, kwa mfano unapotafuta kitu kutoka kwenye kompyuta, kompyuta kabla ya kutekeleza amri hiyo inakuletea tangazo na kukuuliza ya kwamba ni kweli una uhakika wa kutaka kufuta kitu hicho au umefanya hivyo bila kukusudia? pia kompyuta imekuandalia kila kitu unachotaka kukifanya ndani yake kutegemea na malengo yako mwenyewe. Pia kompyuta inazingatiwa ni mwalimu au muelekezaji (Instructor), kwani inakuelekeza jinsi gani unaweza kufanya kazi yako kwa ukamilifu.pia ndani ya kompyuta kuna kitu kinachoitwa kisaidizi (help)mbacho kinatumika kwa ajili ya kufanya utafiti wa kitu fulani ili kufahamu matumizi na njia zake.
Uwezo mkubwa wa kuhifadhi vitu: Miongoni mwa mambo muhimu ndani ya kompyuta ni kupatikana sehemu kubwa ya kuhifadhia vitu kwa amani na bila kupotea vitu hivyo.


Aina za matumizi ya kompyuta.

 Kuna aina kuu tatu za kompyuta, nazo ni kama ifuatavyo:-


1. Kompyuta Dijitali: Ni kompyuta zinazotumika kwa ajili ya kufanyia hesabu pamoja na kazi za kutumia akili.

2. Kompyuta Analogu:Ni kompyuta zinazotumika kwa ajili ya kupokea taarifa (Data) kama zile za kusomea hali ya hewa, kupimia mishipa ya damu na kupimia kiwango cha chumvi kwenye maji.

3. Kompyuta Mahuluti (Hybrid Computers):Kompyuta hizi zinafanana na zile zilizotangulia kutajwa hapo mwanzo, nazo zinatumika kwa ajili ya kutafutia taarifa (Data) kutoka kwa binadamu moja kwa moja na kupitia mandishi na vipimo.

Aina za kompyuta za digitali.

 

Super Computers:Takriban zinapatikana sehemu zote duniani, na zinauwezo na nafasi kubwa ya kuhifadhi vitu vingi (Information) na zinatumika kwa ajili ya kazi za kijeshi na sehemu za ukaguzi, pia kompyuta hizi haziruhusiwi kuhamishwa nje ya nchi na kujua jinsi gani zinatumika. Na zinasifika kuwa na umbile la kati na kati, pia zina uwezo mkubwa na uwepesi wa hali ya juu.

Mainframe Computers:Nazo ni kompyuta zenye umbile kubwa, na zilianza kudhihiri kwake katika mwanzo wa miaka ya hamsini, nazinasifika kwa uwezo mkubwa wa kuhifadhi vitu na pia uwepesi wa hali ya juu.

Mini Computers:Aina hizi za kompyuta zilidhihiri katika kipindi cha miaka ya sitini.Ni kompyuta zenye umbile dogo kuliko zile zilizotangulia kutajwa,na ni bora kwa kuunganishia kompyuta nyengine zinazotumika viwandani na ndani ya nchi.

Micro Computers:Aina hii ya kompyuta inakusanya aina zifuatazo:-
Kompyuta za Kibinafsi(PCs) ambazo ni maalumu kwa ajili ya matumizi ya mtu mmoja tu. Home Computers, Portable Computers: Nazo ni kompyuta za kubeba mkononi, ambazo zimegawanyika katika aina zifuatazo:- 1. Laptop. 2. Notebook. 3. Palmtop.

Kazi za msingi zinazofanyika ndani ya kompyuta.

 

  1. Kazi za uingizaji (Input).
  2. Kazi za uwendeshaji au ufanyishaji (Proccessing).
  3. Kazi za utoaji (Output).
  4. Kazi za kuhifadhi (Storege).

Matumizi ya compyuta.


Elimu:Kutokana na kuendelea kwa elimu ya teknolojia imetusaidia sana kujifunza mambo mbali mbali kupitia kompyuta, ambapo unaweza kutumia kompyuta kwa ajili ya kuuliza maswali na kujibiwa kwa haraka tena kwa njia tofauti, pia unaweza kutumia kompyuta kwa ajili ya kufanya majadiliano ya kielimu, pia unaweza kuandaa vipindi mbali mbali vya masomo na kufundishia elimu tofauti. Pia unaweza kuonyeshea filamu zenye mafundisho mazuri, kama kuonyesha filamu zenye elimu ya jeografia na sayansi ya mifugo na kilimo, kuonyesha sehemu muhimu za nchi yetu, kuonyesha athari za nchi ambazo ndiyo sehemu kuu zinazotuletea fedha za kigeni katika nchi yetu, na kuonyesha picha za maendeleo katika sekta mbali mbali za nchi yetu, pia kuonyeshea mila na tamaduni za taifa letu la Tanzania na mataifa mengine mbali mbali duniani n.k.

Michezo:Kompyuta zimeandaliwa ndani yake programu mbali mbali zenye michezo tofauti, ambayo inaweza kutumika na watu mbali mbali kutofautiana na umri wao, na ambayo inajulikana kama moja ya kazi za kukuza kipaji na kuchangamsha akili, na ni sehemu moja wapo ya kuburudisha nafsi.

Ufundi:Kompyuta zinaweza kutumika kwa ajili ya kufanyia kazi za ufundi, kama kuchora ramani ya nyumba na mazingira ya nje ya nyumba, kutengenezea picha kwa kuibadilisha na kuiremba na kuifanya ionekane katika sura nyengine ambayo tofauti na ile ya asili.

Mawasiliano:Kompyuta inaweza kutumika kwa ajili ya kufanyia mawasiliano kupitia mtandao wa (Internet) ambao leo hii ndiyo umeshika nafasi kubwa sana ya mawasiliano kuliko kitu chengine ulimwenguni, kama kuwasiliana kwa kutumiana ujumbe wa barua pepe (E-mail) ambayo ni rahisi na inafika haraka kuliko barua za kupitia posta, pia kwa kutumia barua pepe hakuna haja ya kufikiria sehemu aliko mtu America au Asia au sehemu nyengine duniani, kuwasiliana kwa maneno ya maandishi (Chat), pia kuwasiliana kwa maneno ya sauti na kuonekana picha.

Usafirishaji:Kwa kutumia kompyuta unaweza kuendeshea kazi za usafirishaji katika vituo vikuu vya usafirishaji, kama usafiri wa ardhini (mabasi, metro na treni), usafiri wa majini (meli), na usafiri wa angani (ndege).

Matumizi ya kiwandani:Kama kuendeshea mashine viwandani kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbali mbali, kama kutengenezea magari, kuzalishia umeme na kutengenezea bidhaa nyengine za kawaida kama nguo mazulia n.k.

Matumizi ya benki:Kama ilivyokuwa ada na kawaida hivi sasa kutumia kompyuta kwa ajili ya kuendeshea kazi za benki,kwa ajili kurahisisha kazi za mahesabu.

Kufanyia matibabu:Kompyuta zimekuwa na matumizi makubwa na muhimu sana katika kufanyia uchunguzi na matibabu hospitalini, kama kuchunguza na kuelekeza dawa ya kutibu ugonjwa uliyoonekana, pia kupimia na kujaribia mimba na kutoa maelekezo kuhusiana na siku na tarehe ya kujifungua.

Kazi za kompyuta.

1. Kuhifadhi vitu (Data):Kama ilivyotanguliwa kusemwa hapo awali kuwa kompyuta ni chombo pekee chenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi vitu, na mpaka hivi sasa bado hakijapatikana chombo chengine chenye uwezo mkubwa wa kuhifadhia vitu zaidi ya kompyuta.

2. kuonyeshea matokeo ya vitu (Data na Information):Kutokana na kuendelea elimu ya teknolojia imeweza kuturahisishia kazi zetu nyingi ambazo tulikuwa tunazifanya kupitia vyombo mbali mbali, na kila chombo kilikuwa na kazi yake maalumu, tofauti na kompyuta ambapo mtu anaweza kuanzisha au kutengeneza kitu na wakati huo huo anaweza kukionyesha kwa kutumia kompyuta yenyewe, yaani kuonyesha ufanisi na sura nzuri ya kitu kilichofanyika.